Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 6, 2023

Tanzania yavuna medali, fedha ndondi Afrika

Na Rahel Pallangyo TANZANIA imevuna medali mbili na kiasi cha Dola za Marekani Dola 15,000 (sawa na Sh milioni 37.2) katika Mashindano ya 21 ya ndondi ya Afrika kwa wanaume na wanawake wakubwa yaliyomalizika jana jijini Yaounde, Cameroon. Grace Mwakamele amekuwa bondia wa kike wa kwanza Tanzania kutwaa medali katika mashindano ya Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili na kupata medali ya fedha na Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh milioni 24.5). Mwakamele alishindwa kwa pointi katika fainali dhidi ya bingwa mtetezi Alicida Panguane wa Msumbuji katika uzito wa Lightmiddle. Bondia wa kiume, Yusuph Changarawe alipata medali ya shaba na kiasi cha Dola za Marekani 5,000 (sawa na Sh milioni 12.4) baada ya kudundwa katika nusu fainali na Nathan Langu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya kuumia juu ya jicho. Mwakamele alifuzu fainali baada ya kumpiga kwa pointi, Seynabou Ndiaye wa Senegal. Akizungumza na gazeti hili Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT), Makori Mashaga alisema timu ya Tanzania iliwakilishwa na wachezaji watatu na imefanikiwa kuliheshimisha Taifa kwa ushindi wa medali mbili moja ya fedha ya Mwakamele na nyingine ya shaba ya Changalawe. Bondia mwingine wa Tanzania, Zulfa Macho yeye alitolewa baada ya kupoteza pambano dhidi ya bingwa wa Cameroon, Ngoune Reine katika uzani wa fly katika hatua ya robo fainali. Mara ya mwisho Tanzania kufanya vizuri katika Mashindano ya Afrika ilikuwa nchini Afrika ya Kusini mwaka 1994. Mashaga alisema kuwa mbali na kuwania zawadi hizo, pia mashindano hayo ni muhimu kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki mashindano ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris, Ufaransa 2024 itakayofanyika Dakar, Senegal baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment