Ndanda wameamua kuifanya Ndanda Day Dar kwa sababu ni sehemu ambayo wana mashabiki wengi ukiachana na Mtwara. Mwaka huu watafanya tamasha hilo mara mbili, kesho litafanyika Dar ambapo watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting lakini watafanya tamasha jingine mkoni kwao Mtwara siku ambayo watacheza na Azam FC ikiwa ni mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.
“Kwa utafiti ambao tumeufanya, klabu ya Ndanda ina mashabiki wengi mkoa wa Dar es Salaam hasa maeneo ya Temeke na Mbagala ndio maana tumeamua kuipeleka Ndanda Day kwenye uwanja wa Chamazi ambao upo karibu na maeneo ya mashabiki wetu,” Peter Simon, mshauri wa masuala ya biashara na masoko Ndanda SC.
Kabla ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting, wachezaji pamoja na viongozi wa klabu hiyo watafanya shghili za kijamii ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwa wagonjwa (wodi ya wazazi) hospitali ya Temeke ambapo watatoa msaada wakishirikiana na wadhamini wao kampuni ya Motisun.
Tamasha hilo litapambwa na wasanii wa Bongofleva wakiongozwa na Jay Moe, TID, Amini na Juma Nature ambao wote wana asili ya Mtwara.
Ndanda inakuwa klabu ya pili baada ya Simba kuadhimisha siku maalumu kati ya vilabu vinavyo shiriki ligi kuu Tanzania bara ambapo wachezaji pamoja na benchi la ufundi hutambulishwa rasmi kwa mashabiki sambamba na jezi zitakazotumika kwa msimu husika.
No comments:
Post a Comment