Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, July 29, 2016

Nyota Medeama asaini miaka miwili Azam FC


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imefanikiwa kunasa saini ya winga nyota wa timu ya Medeama ya Ghana, Enock Atta Agyei, ambaye tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na timu hiyo.
Kinda huyo anatua baada ya kulivutia Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, ambaye amependekeza asajiliwe baada ya kumuona kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Medeama ikiilazimisha sare ya bao 1-1 Yanga katika mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Uongozi wa mabingwa hao umefanya jitihada za hali ya juu hadi kunasa saini yake, ambapo umelazimika kumpandia ndege mshambuliaji huyo hadi mjini Takoradi, Ghana, usajili huo ukiratibiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliyeenda huko na kukamilisha vema kazi hiyo maalumu kwa kuzungumza na pande zote mbili mchezaji na uongozi wa Medeama akiwemo Mmiliki wa timu, Moses Armah.
Akiwa nchini Ghana, Kawemba alipata fursa ya kukutana na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’, Avram Grant raia wa Israel, wakati wa mchezo wa marudiano kati ya Medeama na Yanga ulioisha kwa wenyeji kushinda mabao 3-1.
Katika mazungumzo yake na Kawemba, Grant aliyewahi kuifundisha Chelsea na kuifikisha kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, aliipongeza Azam FC kwa kutambua kipaji cha Enock na kumsajili.
“Nawapongeza sana Azam FC kwa kutambua kipaji cha Enock akiwa amefikisha umri wa miaka 18, nawaahidi nitakuwa namfuatilia kwa karibu kwa kipindi chote cha mkataba wake atakachokuwa Azam FC,” alisema Grant katika moja ya mazungumzo yake na Kawemba.
Enock, 18, mwenye kipaji cha hali ya juu, mara baada ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na Azam FC, anatarajia kutua nchini kesho Jumamosi saa 2.15 asubuhi na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).
Winga huyo mwenye kipaji cha hali ya juu anayetabiriwa kutikisa zaidi miaka michache ijayo, ameanza kung’ara wakati akiwa hana uzoefu mkubwa sana na Ligi Kuu ya Ghana kwani amejiunga na Medeama Desemba mwaka jana baada ya kufanya vizuri akiwa na Windy Professionals ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, hivi sasa ipo kwenye kambi Visiwani Zanzibar ikifanya maandalizi kabambe ya kujiandaa na msimu ujao, kikosi kikiwa chini ya makocha wapya kutoka nchini Hispania.

No comments:

Post a Comment