Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, February 24, 2017

RISALA YA TFF KATIKA UZINDUZI WA BODI YA MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (TFF FOOTBALL DEVELOPMENT FUND).

TANZANIA FOOTBALL FEDERATION

RISALA YA TFF KATIKA UZINDUZI WA BODI YA MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (TFF FOOTBALL DEVELOPMENT FUND).

MH. Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Ndugu Yusuph Singo Mkurugenzi wa Idara ya Michezo.
Ndugu Wajumbe wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu.
Ndugu Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
Sekretariet ya TFF mkiongozwa na Katibu Mkuu Mwesigwa Selestine.
Ndugu Wanahabari.
Wageni waalikwa Mabibi na Mabwana.
Habari za asubuhi.

Ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa pamoja hapa leo.
Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana pamoja na shughuli zako nyingi umeweza kutenga muda wa kuwa na sisi asubuhi hii. Ahsante sana.
Ndugu mgeni rasmi wazo la kuunda hiki chombo lilitujia mwaka 2015 baada ya kuona ugumu wa kutekeleza mipango ya maendeleo kutokana na uhaba wa rasilimali hasa fedha. Hivyo kwa kushirikiana na Rais wa Heshima wa TFF Bwana Leodegar Tenga tuliweza kubuni uanzishwaji wa chombo hiki pamoja na kanuni  za uendeshaji wake. Mfuko huu ulirasimishwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa TFF wa mwaka 2015 na hivyo mfuko huu uko na Katiba ya TFF. Tulifanya hivyo ili kuulinda mfuko huu kutokana na mabadiliko ya uongozi wa TFF ambayo huwa tunayafanya kil baada ya miaka minne.  Kwa mujibu wa Katiba ya TFF kanuni za uendeshaji wa mfuko huu zimeundwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF.
Bodi hii inaundwa na:
Bw. Tido Mhando            -        Mwenyekiti ( Mtendaji Mkuu Azam TV)
Bi. Beatrice Singano        -        Mjumbe (Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel)
Bw. Tarimba Abbas         -        Mjumbe (Mstaafu Bahati Nasibu ya Taifa)
Bw. Salum Rupia             -        Mjumbe (Mkurugenzi NBC)
Bw. Joseph Kahama        -        Mjumbe (Katibu Tanzania/China Friendship
                                                Society)
Bw. Ephraim Mafuru        -        Mjumbe (Mkurugenzi Masoko ILOVO)
Bw. Meshack Bandawe    -        Mjumbe (Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa)
Sekretarieti ya Bodi hii inaongozwa na Mtendaji Mkuu.

Jukumu kubwa la mfuko huu ni kubuni vyanzo mbalimbali vya rasilimali ambavyo vitaliwezesha Shirikisho kutekeleza program zake mbalimbali za maendeleo ya mpira wa vijana na wa wanawake. Mfuko huu unajiendesha kwa uhuru (independently), una akaunti yake benki ambayo inaitwa kwa jina la Mfuko wenyewe na watia saini (Bank Signatories) wanateuliwa na kusimamiwa na Bodi yenyewe.
Kiutaratibu Sekretarieti ya TFF ikiwa na mahitaji itakuwa inatuma maombi kwa maandishi kwenda kwenye Bodi, na Bodi ikijiridhisha na maombi hayo itakuwa inaruhusu matumizi yafanyike kwa masharti kuwa mrejesho wa matumizi hayo uletwe kwenye Bodi kwa kuangalia wadhifa wa wajumbe wa Bodi hii ni dhahiri rasilimali zitakazokusanywa na mfuko huu zitakuwa salama. Ofisi za mfuko huu ziko Mikocheni hapa Dar es Salaam.
Ndugu Mgeni Rasmi,
Kwa kipindi kirefu Tanzania hatujafanikiwa kucheza fainali kubwa za mpira Barani Afrika. Mara ya mwisho kupata mafanikio makubwa kwa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ilikuwa ni mwaka 1980 Tanzania ilipofuzu kucheza fainali za Afrika (AFCON) nchini Nigeria.
Ila kuhakikisha Tanzania inang’ara tena Kimataifa katika mpira wa miguu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linania thabiti ya kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza fainali za kombe la Dunia mwaka 2026 kwa upande wa wanaume (Taifa Stars) na kufuzu kucheza fainali za Dunia kwa mpira wanawake (Twiga Stars) nchini Ufaransa mwaka 2019.
Msingi mkubwa wa mafanikio ya Timu za Taifa duniani kote ni kuwekeza katika mpira wa vijana ili kuhakikisha vijana wanafundishwa mpira kwa kiwango cha Kimataifa kuanzia wakiwa wadogo.  Wakilelewa pamoja na kufundishwa mpira pamoja ukubwani wanaunda Timu ya Taifa imara yenye uwezo wa kushindana na timu yoyote duniani. Hakuna njia ya mkato.
MKAKATI.
Ili kufikia azma hii TFF infanya yafuatayo:

·       Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars).
Mwaka jana Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) ilipata mafanikio makubwa sana kwa kushinda ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Women Challenge). Lengo la TFF ni kuboresha kikosi hiki ili mwaka 2018 kiweze kufaulu kucheza fainali za Afrika kwa mpira wa wanawake nchini Ghana. Timu tatu bora katika fainali hizi zitacheza fainali za Kombe la Dunia la Wanawake nchini Ufaransa mwaka 2019.Ili kutimiza lengo hili kuanzia mwaka jana 2016 TFF ilianzisha Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake. Mwaka huu wa 2017 wachezaji bora 40 toka katika Ligi hii wataingia kambini na kuchujwa ili wale walio bora waongezwe kwenye kikosi cha sasa cha Twiga Stars ili kuiimarisha. Timu itaendelea kuwa inaingia kambini na kupewa mechi za majaribio. Tunaamini kwa mkakati huu Tanzania itafuzu kucheza fainali za Afrika 2018 na za Dunia 2019.
          Serengeti Boys.
Hii ni timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17. Kikosi cha sasa cha Timu hii ni cha vijana waliozaliwa baada ya tarehe 01 Januari, 2000.  Kikosi hiki kilikusanywa pamoja kwa mara ya kwanza mwaka 2014 kutokana na mashindano ya Copa CocaCola na Airtel Rising Stars, tunawashukuru sana AIRTEL ambao wameendelea kuwa karibu na timu hii. Hadi sasa timu hii imesafiri na kuweka kambi nchi mbalimbali duniani zikiwemo Madagascar, Seychelles, Rwanda, India na Korea ya Kusini. Hadi sasa kikosi hiki imecheza mechi 12 za Kimataifa dhidi ya timu kubwa za Taifa ikiwemo ya Marekani, Korea ya Kusini na Afrika Kusini na kimefanikiwa kushinda mechi saba, sare tatu na kufungwa mechi mbili tu.
Ni jambo la fahari kubwa kwa Taifa letu kuwa Serengeti Boys imefuzu kucheza fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17. Fainali hizi zitafanyika nchini Gabon kuanzia tarehe 21 Mei hadi tarehe 04 Juni, 2017.Katika fainali hizi timu nane zitashiriki na zimegawanywa katika makundi mawili ambayo ni kundi A ni Gabon, Ghana, Cameroon na Guinea ya Conakry. Kundi B ni Tanzania, Angola, Mali  na Niger. Timu mbili bora kila kundi zitafaulu kucheza fainali za Kombe la Dunia India mwezi Novemba.
Maandalizi ya Serengeti Boys kuelekea Gabon yatahusisha kambi za ndani na za nje ya nchi. Tunakadiria kuwa ili tushiriki kwa mafanikio katika fainali hizi jumla ya fedha zilizopungua ni Shs. 1,000,000,000/=( Billioni moja) zitahitajika ili kulipia gharama za kambi ndani na nje ya nchi.
Tutaendelea kuilea kikosi hiki ili mwaka 2019 kiweze kufaulu kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 (Afcon U-20).

·        Fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Tanzania imepewa fursa na Shirikisho la Mpira Barani Afrika CAF ya kuwa wenyeji wa Fainali za Afrika kwa vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 (Afcon U-17). Hii ni heshima kubwa sana kwa Tanzania na itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupata uenyeji huu tangia tupate uhuru. Fursa hii tukiitumia vyema itatupatia mwanya mzuri wa kunyakua ubingwa wa Afrika tukiwa wenyeji wa michuano. Aidha kufanikisha kuandaa mashindano haya makubwa kutafungua njia kwa Tanzania kuandaa fainali za Afrika kwa wakubwa (Afcon) kwa miaka ya baadae.
Maandalizi ya fainali hizi kama wenyeji yana sehemu mbili kubwa:
Ya kwanza, ni maandalizi ya mashindano yenyewe ambayo ni pamoja na kuandaa viwanja kwa kiwango stahiki, kuandaa hoteli za kutosha kwa ajili ya malazi ya washiriki, kuandaa miundo mbinu ya mawasiliano, maandalizi ya itifaki nk. Hii inahitaji kuunda Kamati ya Taifa ya Maandalizi (Local Organizing Committee). Taratibu za kuunda kamati hii zinaendelea.
Ya pili, ni maandalizi ya Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (U17) itakayoshiriki fainali hizi. Kama wenyeji Tanzania itaingia moja kwa moja kwenye fainali hizi. TFF ilianza maandalizi ya timu hii mwaka 2014 ambapo yalifanyika mashindano ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 13 wakati huo. Vijana 22 bora toka katika mashindano hayo walikusanywa na kuwekwa pamoja katika shule ya kukuza na kulea vipaji vya wanamichezo ya Alliance Mwanza ambapo wamekuwa wakisoma na kufundishwa mpira. TFF inalipia gharama za masomo ya vijana hawa. Tarehe 18 Disemba, 2016 timu hii (ambayo sasa  ni ya vijana umri chini ya miaka 15) ilicheza mechi yake ya kwanza ya Kimataifa dhidi ya Burundi na kushinda kwa bao 3-2. Utaratibu huu utaendelea na kikosi kitazidi kuboreshwa.
            Fainali za Olimpiki mwaka 2020 Tokyo.
TFF imejizatiti kuhakikisha timu yetu ya Taifa umri chini ya miaka 23 (Kilimanjaro Warriors) inafaulu kucheza fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020.Ili kutimiza lengo hili TFF ilichezesha Ligi ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20 mwaka jana. Hawa ni wale waliozaliwa baada ya tarehe 01 Januari, 1997. Mwezi Januari mwaka huu vijana 40 bora toka katika ligi hii waliitwa kambini na kuchujwa ili wabaki vijana 22 wakakaoanza kambi maalum kujiandaa na kufuzu kucheza fainali za Olimpiki. Tanzania haijawahi kufuzu kucheza mpira wa miguu katika fainali za Olimpiki. Safari hii tumedhamiria tufuzu. Tuna imani kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania TOC tutaweza kufikia athma  hii.
           Kuelekea Kombe za Dunia 2026.
Matumaini ya TFF ni kuwa muunganiko wa wachezaji bora tokana na Fainali zaa Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019, Serengeti Boys ya sasa na Kilimanjaro Warriors ( Timu ya Olimpiki) iliyoundwa mwaka huu yatalipatia Taifa letu fursa ya kuunda kikosi imara cha timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo itaanza kuonyesha makali yake Afrika na Duniani kuanzia mwaka 2021 katika kuelekea fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Kwa kuwa program zote hizi zinahitaji matumizi makubwa ya fedha ikiwemo kugharamia kambi, usafiri wa ndani na wa nje ya nchi kwa mechi za majaribio na kununua vifaa vya michezo ni matumaini ya TFF kuwa kwa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu yakiwemo Mashirika na Makampuni ya umma na binafsi, taasisi mbalimbali na watu binafsi wataweza kuchangia maendeleo ya mpira wa miguu kwa kupitia mfuko huu.Tunaomba Serikali itushike mkono katika jambo hili.
Ndugu mgeni rasmi kama ishara ya kutuzindulia Bodi ya Mfuko huu tutaomba uwakabidhi wajume wa Mfuko huu Katiba ya TFF, Kanuni za uendeshaji wa mfuko.
Ahsante sana.
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ubariki Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania.
Jamal Malinzi
DAR ES SALAAM
23 Februari,2017

No comments:

Post a Comment