Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, March 14, 2015

TFF WAAMUZI HAWA HAMWATENDEI HAKI



     Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamali Malinzi (kulia) akimkabdishi Florentina Zablon beji ya FIFA mapema Januari mwaka huu.
“KUPATA beji ni kitu kingine na kukaa nayo ni jambo lingine.” Nimenukuu maneno ya mwamuzi
wa kimataifa wa Tanzania, Israel Mujuni Nkongo ambayo aliyasema wakati wakikabidhiwa beji za FIFA
na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwenye ofisi za shirikisho hilo zilizopo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Maneno hayo ya Nkongo aliyatoa alipohojiwa na waandishi wa habari kwani yeye ndiye alikuwa mwamuzi mkongwe kuliko wote kwenye hafla hiyo iliyofanyika Januari 6, mwaka huu.

Katika hafla hiyo, Malinzi alikabidhi waamuzi 18 wa Tanzania beji za FIFA, ambazo ni kiashirio (kitambulisho) cha kutambuliwa na shirikisho hilo la soka la kimataifa. Katika waamuzi 18, wa kike ni saba,
watatu wakiwa ni wa kati ambao ni Jonesia Kabakama, Florentina Chief na Sophia Mtongori huku waamuzi wasaidizi wakiwa ni Dalila Mtwana, Grace Wamala, Hellen Joseph Mduma na Kudura Omary Maurice.
Kwa upande wa wanaume, waamuzi wa kati ni Nkongo, Martin Sanya, Mfaume Ali Nassoro na Waziri Sheha Waziri huku waamuzi wasaidizi ni Alli Kinduli, Ferdinand Chacha, Frank Komba, John Kanyenye,
Josephat Bulali, Samuel Mpenzu na Soud Lila.

Kabla sijazama zaidi kwenye makala haya, naomba ieleweke kuwa mimi ni mwamuzi daraja la kwanza na ninachokiandika nakielewa kulingana na ufahamu wangu pia nakubali kukosolewa, kushauriwa pia kuelekezwa.

Kulingana na kanuni za FIFA, mwamuzi akishapata beji analazimika kuivaa kwenye michezo yote ambayo inaendeshwa na mwanachama wa FIFA, hapa namaanisha TFF hivyo mwamuzi anatakiwa kuvaa hiyo beji
iwe kwenye ligi ya wilaya, mkoa, daraja la kwanza au Ligi Kuu.
Katika ligi zinazoendelea Tanzania nimeona waamuzi wawili wa kike ambao wana beji za FIFA zinazowatambua kama waamuzi wa kati, wakichezesha kama waamuzi wasaidizi, jambo ambalo limenipa maswali hadi yakanisukuma kuandika makala haya.

Tunashukuru kupata waamuzi wengi wa kike, kwani ni mara ya kwanza kupata waamuzi saba kwa wakati mmoja na hii inadhihirisha kuwa soka la wanawake Tanzania limepiga hatua. Mwaka jana Tanzania haikuwa
na beji yoyote ya FIFA kwa upande wa wanawake ila mwaka huu tunazo saba, hivyo sasa ni wakati wetu wa kuzitunza na kuzitumia.

Mwanzoni nilianza kwa kunukuu maneno ya Nkongo ambayo yalinipa tabu kudadavua ana maana
gani, kusema vile ilhali yeye pia ni mwamuzi, lakini sasa naanza kuelewa alichomaanisha.
Nimeona ratiba ya ligi daraja la kwanza na Ligi Kuu nikaona majina ya Florentina Zablon Chief na Sophia Ismail Mtongori wamepangwa kwenye ratiba, lakini wanachezesha kama waamuzi wasaidizi wakati
wao beji zao zinawatambua kama waamuzi wa kati.

Jambo hili lilinifanya nikumbuke maneno ya Nkongo aliyosema kuwa kupata beji ni jambo lingine na kukaa nayo pia ni kitu kingine kwani hapa hao wanaopanga ratiba za ligi na kumpanga mwamuzi wa kati mwenye
beji ya FIFA kucheza kama mwamuzi msaidizi hawamsaidii, bali wanachangia kurudisha kiwango chake kuwa duni.
Maneno ya Nkongo hata kama hayakumaanisha haya yanayotendeka kwa hawa waamuzi wawili lakini yanadhihirisha wazi kukaa na hizi beji itakuwa kazi kwani endapo mwamuzi anachezeshwa kwenye nafasi ambayo hastahili kucheza ni sawa na mamlaka inayopanga ratiba inachangia kuwapokonya beji zao.
Tangu nianze kuwaona waamuzi wa kike wenye beji sijawahi kuona mwamuzi wa kati akicheza kama mwamuzi msaidizi hili nimeliona kwenye uongozi wa sasa wa TFF ambao wanasema wanataka waamuzi wa kike wa Tanzania wakachezeshe fainali zijazo za Afrika na za dunia pia.

Beji ya kwanza kwa wanawake ilikuwa ya Flora Kashaija, akaja Isabela Kapera na mwishoni ilikuwa Judith Gamba, wote hawa walichezesha Ligi Kuu kama waamuzi wa kati na walifanya vizuri tena mechi ambazo
zilisemekana ngumu lakini nashangaa kuona Chief na Mtongori wanacheza kama waamuzi wasaidizi.
Najiuliza hivi kweli hawana uwezo wa kupiga filimbi dakika 90 hadi 120 na mchezo ukamalizika na timu zikatoka uwanjani kila mmoja akiwa ameridhika na matokeo?
Kwani mnawachezesha kama waamuzi wasaidizi, kuna siri gani imejificha? Tena labda hili hamjaliona mnawanyong’onyesha kwa sababu hawavai beji zao kwa vile nafasi wanazocheza sio walizopewa beji.

Baadhi ya waamuzi wa Tanzania wenye beji za FIFA wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye Uwanja wa kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi wa kike wa kimataifa (FIFA) Florentina Zablon (kulia) akiwa na waamuzi wenzake pamoja na
manahodha wa Simba na Yanga wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa wiki iliyopita
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Florentina ana beji ya FIFA inayomtambua kama mwamuzi wa kati lakini kwenye ligi za nyumbani anapangwa kucheza kama mwamuzi msaidizi.

Kila siku wanamwona Kabakama anachezesha kwenyenafasi yake lakini wao hawachezi naamini kabisa kibinadamu inawajengea chuki kwani wanadhani wanaonekana hawawezi lakini mwenzao anaweza.
Labda kama mnaweza kusema kuna sababu ya msingi ya kufanya hivyo jambo ambalo naamini hakuna,
huenda mliwapa beji za kwenda kukaa sandukuni wakati mwenzao anaivaa yake na huenda mwaka
ukamalizika asiivae kwani hakupata mechi ya kimataifa, jambo ambalo siombei litokee.

Huyu mwamuzi unayemchezesha kama mwamuzi msaidizi msimu mzima mfano leo hii anapata mechi ya CAF au FIFA kwa vile beji yake ni mwamuzi wa kati anatakiwa akachezeshe mchezo wa kufuzu fainali za Afrika kwa upande wa wanawake kati ya Nigeria na Afrika Kusini, hivi akienda kufanya vibaya anayestahili lawama ni yeyeau nchi?

Kulingana na sheria za soka, sheria namba tano inamzungumzia mwamuzi wa kati, madaraka na majukumu yake. Kwenye madaraka mwamuzi ana madaraka saba na majukumu 11 ambayo yote anatakiwa
kuyafanya kwenye mchezo na pia sheria namba sita ambayo ni mahususi kwa mwamuzi msaidizi inamtaka atekeleze kazi saba tu akiwa mchezoni.

Kwa kufikiria haraka haraka huyo mwamuzi ambaye anatumika kama mwamuzi msaidizi na kumfanya
asivae beji yake ambayo inaongeza umaridadi akiwa uwanjani au mchezoni, amezoea kumsaidia mwamuzi wakati wa mchezo kwa kuonesha mpira uliotoka uwanjani, kuonesha upande gani mpira uliotoka urushwe au pigo la kona, kukamata mchezaji aliyeotea kuonesha au kuashiria mchezaji anapotaka kuingia baada ya mwamuzi wa akiba kumkagua na mwisho makosa yanayotokea uwanjani yaliyopo kwenye umbali usiozidi mita 9.15.

Sasa amepangwa na CAF akachezeshe mechi akiwa uwanjani anatakiwa atekeleze kazi 18 wakati yeye amezoea kutekeleza kazi saba tu, hivi akikamata offside atakuwa amekosea? Binafsi sioni ajabu kwa vile mazoea hujenga na kwa vile amezoea kumsaidia mwamuzi inakuwa ngumu kukumbuka leo yeye hachezi kama mwamuzi msaidizi badala yake yeye ndio mwamuzi.

Mashabiki na kamisaa watamshangaa huyo mwamuzi na kila mtu watamjadili kwa maoni yake maana wengine wanaweza kusema hajui, wengine watasema wanachojua wao kumbe tatizo limetokana na kumchezesha nafasi ambayo hajazoea. Hii ni rahisi kueleweka kwa mfano mchukue mchezaji anayecheza
nafasi ya beki halafu umwambie acheze kama mshambuliaji, naamini hataweza badala yake inawezekana
akapokea mpira vizuri badala ya kufunga bao akapiga kuondoa eneo la hatari akidhani wanashambuliwa
wao kumbe wao ndio wanashambulia.

Malinzi kama kweli nia yako ni dhahiri kuwa waamuzi hawa wachezeshe fainali za wanawake Afrika na fainali zijazo za Dunia, wapangeni nafasi zao ili kujenga mazoea ya kutumia mamlaka na madaraka wakati wa mchezo na kupata uzoefu ili isije ikawa tumepata beji ambazo baada ya mwaka mmoja zitaondoka kutokana na uchezeshaji duni.

Mwisho naamini kamati ya waamuzi ina wajumbe makini ambao wote ni wamuzi wastaafu na baadhi yao wamechezesha hadi mechi za kimataifa hivyo wanajua fika mwamuzi anatakiwa acheze nafasi ya beji anayomiliki. Kamati ya waamuzi Katibu wake Charles Ndagala ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) amewahi kuwa mwamuzi msaidizi wa Kimataifa, kama inawezekana mwamuzi wa kike mwenye beji ya FIFA inayomtambua kama mwamuzi wa kati kuchezeshwa kama mwamuzi msaidizi
kwanini hili lisifanyike hata kwa waamuzi wa kiume?

Tuondoe ile dhana ya kuwa wengine wanaweza lakini wengine hawawezi na kama TFF hamjaliona hili basi mimi nimewasemea leo, fungueni macho muone mchukue hatua tuache kudharau vitu ambavyo vitatuletea madhara hapo baadae ili tusitafute mchawi kumbe mchawi ni sisi wenyewe.
Vinginevyo hakukuwa na maana ya kupendekeza majina yao katika orodha ya waamuzi wanaostahili
kupewa beji na hatimaye wamezipata lakini hawazivai na kuzitumia katika nafasi zao.

No comments:

Post a Comment