Timu nne vinara wa Ligi Daraja la Pili kutoka makundi manne,
zinatarajiwa kuanza kupambana keshokutwa Jumatano - Machi mosi, mwaka
huu ‘Play off’ kutafuta timu Tatu Bora, zitakazopanda daraja kucheza
Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018.
Timu hizo zilizofanya vema ni pamoja na JKT Oljoro ya Arusha,
Cosmopolitan ya Dar es Salaam, Mawenzi ya Morogoro na Transit Camp ya
Shinyanga. Ziliibuka vinara katika makundi yao.
Ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, inaonesha kuwa Ratiba ya Nne Bora
itakuwa na raundi mbili ambazo kwa pamoja zitacheza kwa mwezi mmoja
kuanzia Machi mosi hadi Aprili mosi, mwaka huu.
Raundi ya kwanza itaanza siku ya Machi mosi, mwaka huu ambako
kutakuwa na mechi mbili ambazo Transit Camp itacheza na Mawenzi kwenye
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati Cosmopolitan itacheza na JKT
Oljoro kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Machi 5, mwaka huu kutakuwa pia na michezo
miwili ambako JKT Oljoro itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Mawenzi Market itacheza
Cosmopolitan kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Machi 12, mwaka huu JKT Oljoro itacheza na Mawenzi Market kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Cosmopolitan itacheza
na Transit Camp kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Raundi ya Pili ya ligi hiyo, itaanza Machi 18, mwaka huu kwa timu za
Mawenzi Market itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro wakati siku hiyo, JKT Oljoro itacheza na Cosmopolitan katika
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Machi 25, mwaka huu Cosmopolitan itapambana na Mawenzi Market kwenye
Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam ilihali Transit Camp
itacheza na JKT Oljoro Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Funga dimba la hatua hiyo, itakuwa Aprili mosi, mwaka huu kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako Mawenzi itakuwa mwenyeji wa JKT
Oljoro wakati Cosmopolitan itakuwa mgeni wa Transit Camp kwenye Uwanja
wa Kambarage, Shinyanga.
No comments:
Post a Comment