SIMBA imekuja na
mfumo mpya wa mazoezi, uliobatizwa jina la 'Simba Luku', ambao una lengo la
kuwafanya wachezaji kuongeza bidii ya mazoezi.
Kocha Msaidizi wa
Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ndiye aliyeubuni mfumo huo, akiufananisha na
mita za Luku, ambazo mtumiaji hulipia umeme kadri anavyotumia.
Julio anamaanisha
kwamba kuanzia sasa wachezaji wanatakiwa kujituma zaidi ili walipwe posho nzuri
zaidi na kuweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Kocha Mkuu wa
Simba, Abdallah Kibaden, amelifafanua kwamba kwa kupitia mfumo huo,
kikosi cha vijana wake kinaweza kuwa na ushindani mkubwa wa namba, kwani kila
safu ina wachezaji zaidi ya watatu wanaochuana.
Kwa mujibu wa
Kibadeni, mchezaji anatakiwa kujituma vilivyo ili aweze kujihakikishia namba na
maslahi zaidi.
"Hilo jina
halijakosewa kabisa, maana ushindani uliopo katika kikosi changu ni mkubwa,
kama ilivyo kwa mita za Luku, huwezi kupata umeme hadi uingize fedha na hivi
ndivyo itakavyokuwa kwa wachezaji wetu, kwani hawataweza kupata nafasi hadi
wajitume zaidi mazoezini," alisema Kibadeni.
Kibadeni pia
amesema kwamba ameongeza zaidi dozi ya mazoezi kwa vijana wake, ambapo sasa
timu itakuwa ikijifua mara mbili, asubuhi na jioni.
Tangu ianze
mazoezi juzi Jumatatu, ilikuwa ikifanya mazoezi mara moja kwenye Uwanja wa
Kinesi, jijini Dar es Salaam, lakini kuanzia leo Jumatano, Kibadeni ameamua
kuwaongezea dozi wachezaji wake.
Kibadeni amelazimika
kuongeza mazoezi kutokana na kuweka nia ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu na
kuijenga timu kwa stamina zaidi.
Akizungumzia
maandalizi yake ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, itakayochezwa Septemba 14 mwaka
huu, Kibadeni alisema kwamba hawezi kuanika mbinu atakazotumia, lakini kwa
jinsi timu yake ilivyojipanga anaamini watashinda.
No comments:
Post a Comment