WAZIRI SANGU APONGEZA NSSF KWA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI NCHINI KENYA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu  (wa pili kutoka kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Mbunifu wa Majengo na Msimamizi wa Mradi, Bw. Albert Mwambafu (kushoto) kuhusu ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipotembelea mradi huo kukagua maendeleo ya ujenzi wake tarehe 9 Novemba, 2026, Jijini Nairobi, Kenya. Kulia ni Mkurugenzi wa NSSF, Bw. Masha Mshomba.

✅Amesema mradi huo utachagiza kukuza uchumi na thamani ya Mfuko

✅Asisitiza Mradi ukamilishwe kwa wakati

Na  Mwandishi Wetu - Nairobi, KENYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuwekeza katika mardi wa kimkakati wa jengo la kitega uchumi nchini Kenya ambalo litachagiza kukuza thamani ya uwekezaji wa Mfuko huo na shughuli za kiuchumi.

“Mradi huu unaotekelezwa katika eneo la kimkakati la takribani ekari mbili ndani ya jijini Nairobi utakapokamilika utaongeza thamani ya uwekezaji kwa Mfuko wa NSSF, kukuza shughuli za kiuchumi na kuwezesha Tanzania kutangaza zaidi vivutio vyake vya utalii,” amesema

Mhe. Sangu ametoa pongezi hizo leo Novemba 9, 2026 alipokuwa katika ziara ya kikazi jijini Nairobi iliyolenga kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi unaotekelezwa kwa ubia kati ya Mfuko wa NSSF na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aidha, amesisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuelekeza uwekezaji katika maeneo yenye tija na yanayokuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Kadhalika, ameutaka Mfuko wa NSSF pamoja na mkandarasi wa mradi huo kuendeleza kasi ya ujenzi ili kukamilisha mradi kwa wakati uliopangwa mwezi Juni, 2028. Pia, amesisitiza suala la usimamizi na udhibiti wa ongezeko la gharama za utekelezaji ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha za Serikali inafuatwa.

Akizungumza kwa naiba ya Balozi, Mtawala Mkuu Bi. Herieth Magogo amesema mradi huo ni uwekezaji mkubwa na ni sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya Tanzania inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya.

Ameongeza kuwa, Kenya ni miongoni mwa wadau wakubwa wa Tanzania katika sekta za biashara na uwekezaji, hivyo utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu inayoonesha dhamira ya nchi hizo mbili kuendeleza ushirikiano wenye manufaa ya pamoja, pamoja na kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Bw. Masha Mshomba amesema kuwa uwekezaji huo ni wa kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza mfuko huo umewekeza nje ya mipaka ya Tanzania.




Amesema uamuzi huo umetokana na ukuaji mkubwa wa NSSF katika miaka ya hivi karibuni, hivyo kuhitaji kupanua zaidi shughuli zake za uwekezaji ili kuendana na mahitaji na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni. 

“Uwekezaji huo wa kimkakati nje ya Tanzania ni mpango muhimu utakaoiwezesha NSSF kuongeza wigo wa uwekezaji, kukuza mapato na kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa,” amesema 

Kwa upande wake, Mbunifu wa Majengo na Msimamizi wa Mradi huo, Bw. Albert Mwambafu, amemhakikishia Mheshimwa Waziri kuwa mradi huo utakamilika kwa ubora uliokusudiwa na kuwa alama muhimu ya mafanikio ya Watanzania katika sekta ya usanifu majengo na usimamizi wa miradi mikubwa nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa upande mwengine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, mara baada ya kukagua mradi huo ametembelea ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Jijini Nairobi, nchini Kenya.


No comments