RAIS SAMIA AAGANA NA BALOZI WA AFRIKA KUSINI, AKUTANA NA MWEKEZAJI WA QATAR IKULU



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Novemba 6, 2026, ameagana na Balozi wa Afrika Kusini nchini, Mheshimiwa Noluthando Mayende-Malepe, anayemaliza muda wake wa utumishi wa kidiplomasia.

Katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam., Balozi Mayende-Malepe amemshukuru Rais Dkt. Samia, Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa na ukarimu aliooneshwa katika kipindi chote cha utumishi wake. 

Ameeleza kuwa uhusiano wa kindugu na kihistoria baina ya Tanzania na Afrika Kusini, uliojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, uliifanya kazi yake kuwa ya kipekee na yenye mafanikio.  

Balozi huyo amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa nchi aliyoifurahia zaidi kuhudumu katika kazi zake za ubalozi na anaondoka akiwa na kumbukumbu nzuri. 

Aidha, amepongeza mchango wa Tanzania katika kuimarisha masuala ya kikanda na kimataifa, huku akizikaribisha kampuni nyingi zaidi za Kitanzania kwenda kufanya biashara na kuwekeza nchini Afrika Kusini. 

Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amempongeza Balozi Mayende-Malepe kwa kuhitimisha vyema utumishi wake wa miaka minne tangu alipowasilisha hati zake za utambulisho Agosti 25, 2022. 

Rais Samia amebainisha kuwa katika kipindi cha uongozi wa balozi huyo, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kimeongezeka, na akahimiza kuendelea kutumika kwa fursa zilizopo ili kukuza zaidi biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili.  


 

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa kampuni ya Thirty-Five Investment Holding ya nchini Qatar, Dkt. Khalid bin Mohammed bin Abdullah Al Attiyah, ambaye ameeleza dhamira ya kampuni yake kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za kimkakati.  

 Dkt. Al Attiyah amebainisha kuwa kampuni hiyo imevutiwa kuwekeza katika sekta ya kilimo na ufugaji, hususan katika uzalishaji wa sukari na ufugaji wa ng'ombe katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma. 

Vilevile, wamejadili fursa za uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu pamoja na ujenzi wa mitambo ya uchakataji na miundombinu ya kuhifadhi samaki katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa.   Mbali na Tanzania Bara, mwekezaji huyo amesema kampuni yake inafanya tathmini ya kuwekeza katika miundombinu ya usafiri visiwani Zanzibar, ambako tayari wataalamu wake wameanza majadiliano ya awali na taasisi husika.   

Akihitimisha mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia amezitaka taasisi zote za serikali zinazohusika kuendeleza mazungumzo hayo na kampuni hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuhakikisha fursa hizo zinaendelezwa kwa tija na manufaa ya pande zote mbili.   

No comments