Dkt. Samia awasili Jijini Addis Ababa kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 22 Novemba, 2026 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili.
Alilakiwa na Waziri wa Ubunifu na Teknolojia wa Ethiopia, Mhe. Frehiwot Tamiru na watoto wa Kitanzania wanaoishi nchini humo.
Akiwa Addis Ababa, Mhe. Rais Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), ambao unaandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Ethiopia pamoja na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kuanzia tarehe 23 hadi 27 Novemba, 2026
Mkutano huo unatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 30,000 ana kwa ana na mtandaoni.
Mkutano wa CPHIA 2026 unawakutanisha viongozi wa serikali, watunga sera, wanasayansi na wataalamu wa afya kujadili vipaumbele vya afya ya umma barani Afrika, ukilenga kuimarisha ufadhili wa ndani wa sekta ya afya, kupanua uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya bara na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.
Tarehe 23 Novemba, 2026, katika ufunguzi rasmi wa mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Addis, Rais Samia—ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Mama na Mtoto—atazindua Mpango Elekezi wa Kinara wa AU kuhusu Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto na Kijana Balehe (2026–2030).
Mpango huo unalenga kupata ridhaa ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutekeleza malengo ya "Sifuri Tatu" kupitia mipango na bajeti za kitaifa za afya katika nchi zote 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, ukiwa na huduma za afya ya msingi kama msingi wa utoaji huduma.
Mpango huo wa mwaka 2026 hadi 2030 unalenga kuunga mkono nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia malengo matatu ya pamoja ya Sifuri Tatu. Lengo la kwanza ni Sifuri Kujifungulia Nyumbani ili kuhakikisha kila uzazi unahudhuriwa na wataalamu wenye ujuzi wa afya katika kituo cha afya chenye vifaa stahiki, upatikanaji wa wakati wa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga, na mfumo thabiti wa rufaa.
Lengo la pili ni Sifuri Vifo Vinavyoweza Kuzuilika vya Mama na Mtoto Mchanga kupitia kuimarisha ufuatiliaji na mwitikio wa vifo vya uzazi na watoto wachanga ili kubaini sababu na mapungufu, kuchukua hatua za kurekebisha, na kufuatilia utekelezaji wake, huku lengo la tatu likiwa ni Sifuri Watoto Wasiopata Chanjo ili kuhakikisha kila mtoto anafikiwa na kulindwa kwa chanjo kulingana na umri wake, hasa katika maeneo ya pembezoni na yasiyofikiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa Mpango Elekezi, Afrika inachangia takriban asilimia 70 ya vifo vyote vya akina mama duniani, huku uwiano wa vifo vya uzazi barani humo ukikadiriwa kufikia vifo 442 kwa kila vizazi hai 100,000, wakati lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni kushusha uwiano huo chini ya 70 ifikapo mwaka 2030.
Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua ndiyo sababu kuu ya vifo vya akina mama katika nchi nyingi za Afrika, huku uzito pungufu/kuzaliwa kabla ya wakati na matatizo yanayohusiana na wakati wa kujifungua yakiwa sababu kuu kwa watoto wachanga, na zaidi ya nusu ya watoto wote duniani waliokosa chanjo katika mwaka wao wa kwanza wa maisha wakiwa barani Afrika.
Kwa upande wa Tanzania, takwimu zinaonyesha maendeleo makubwa katika sekta hiyo, ambapo uwiano wa vifo vya uzazi umepungua kutoka 556 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022, huku asilimia ya wanaojifungulia katika vituo vya afya ikiongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2010 hadi asilimia 81 mwaka 2022.
Vilevile, asilimia ya waliohudumiwa wakati wa kujifungua na wataalamu wenye ujuzi wa afya iliongezeka kutoka asilimia 49 mwaka 2010 hadi asilimia 85 mwaka 2022, vituo vya afya vinavyotoa huduma jumuishi za dharura za uzazi na mtoto mchanga vimeongezeka kutoka 115 mwaka 2015 hadi takriban 630 mwaka 2026, na vitengo vya huduma jumuishi za watoto wachanga vimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2026.
Mpango huo pia unatambua mchango wa kampeni ya kitaifa ya "Jiongeze Tuwavushe Salama" iliyozinduliwa na Dkt. Samia mwaka 2018 akiwa Makamu wa Rais, pamoja na mchango wa mfumo wa m-Mama katika kuimarisha usafiri wa dharura na rufaa, upanuzi wa huduma za dharura kwenye vituo vya afya, na uimarishaji wa ufadhili wa moja kwa moja wa vituo vya afya.
Baada ya kuteuliwa kuwa Kinara wa Afya ya Mama na Mtoto wa Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliofanyika Addis Ababa mwezi Februari 2026, Rais Samia atahamasisha uongozi wa kisiasa katika nchi wanachama, huku Sekretarieti ya Kinara ikifuatilia ahadi na utekelezaji, Africa CDC ikiratibu msaada wa kitaalamu, Kadi ya Alama ya Viashiria Saba ya Rais ya RMNCAH ikifuatilia maendeleo, na tathmini ya katikati ya kipindi ikifanyika mwaka 2028 ili kuweka msingi wa pamoja wa kufikia malengo ya Sifuri Tatu ifikapo mwaka 2030 katika nchi zote 55 wanachama.





Post a Comment