RAIS SAMIA AWATUNUKU KAMISHENI NA SHAHADA MAAFISA WANAFUNZI TMA MONDULI




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 21 Novemba 2026 amewatunuku kamisheni na shahada maafisa wanafunzi wa Kundi la 07/23 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na Kundi la 73/25 Regular, katika uwanja wa gwaride wa Jenerali JJ Mkunda uliopo Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli, mkoani Arusha.

Tukio hilo limeenda sambamba na Mahafali ya Saba ya Shahada ya Sayansi ya Kijeshi kwa maafisa wanafunzi wa kundi hilo la 07/23, ambapo baada ya kuwasili chuoni hapo, Rais Dkt. Samia alisalimiana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, kabla ya kupokea Salamu ya Rais na kufuatiwa na heshima ya Wimbo wa Taifa.

Katika ratiba hiyo ya kijeshi, Amiri Jeshi Mkuu alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na maafisa wanafunzi hao, ambapo pia gwaride hilo lilipita mbele yake kwa mwendo wa pole na wa haraka kutoa heshima kabla ya kutunukiwa rasmi kamisheni na shahada zao.

Baada ya kutunukiwa kamisheni na shahada hizo, maafisa hao wapya walivalishana vyeo na kuapa Kiapo cha Utii mbele ya Amiri Jeshi Mkuu, kabla ya kushiriki picha ya pamoja na Rais Dkt. Samia, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, CDF Jenerali Jacob John Mkunda, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).




















No comments