RAIS SAMIA AHIMIZA UTEKELEZAJI WA DHANA YA POLISI JAMII
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kupanua wigo wa Polisi Jamii ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuimarisha imani yao kwa Jeshi hilo.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo, tarehe 20 Novemba, 2026, akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi katika Shule ya Polisi, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Akirejea ushirikiano wa polisi na wananchi katika kata na shehia zote nchini, Rais Dkt. Samia amewataka askari kuyafikia makundi yote ya jamii katika maeneo yao kutoa elimu kuhusu amani, usalama na utii wa sheria.
"Tunataka wananchi wawe na imani na Jeshi la Polisi," amesema Rais Dkt. Samia akieleza lengo la kuimarisha mahusiano hayo na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada za kushirikisha wananchi katika ulinzi wa amani na utulivu nchini.
Katika hilo, ameonya juu ya mwenendo na tabia za Maafisa na Askari wachache wasio waadilifu, akitahadharisha kuwa mwenendo huo unadhoofisha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini katika kuchunguza usambazaji na matumizi ya vilevi kwa wanafunzi shuleni.
Vilevile, ameelekeza ukamilishaji wa Mradi wa Miji Salama (Safer Cities) itakayotumia teknolojia za kubaini ukiukwaji sheria za barabarani ili kudhibiti ajali, sambamba na kuhimiza mafunzo kwa watumiaji wa barabara, hususan maafisa usafirishaji (bodaboda).
Rais Dkt. Samia pia amehusisha wajibu wa Jeshi la Polisi kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akihusianisha utekelezaji wake na hali ya nchi kuendelea kuwa na amani na usalama, unaoipa sekta binafsi imani ya kuongeza uwekezaji zaidi nchini.
Akiwasilisha tathmini ya hali ya nchi katika mkutano huo, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia sita mwaka 2025, akibainisha kuwa Serikali inatarajia kuongeza ukuaji huo kufikia asilimia 6.3 hadi 6.5.
Katika siasa, Rais Dkt. Samia amesema Serikali inaendelea kutekeleza hatua za mashauriano na makundi tofauti ya wadau kuelekea uundwaji wa Tume ya Maridhiano, itakayotengeneza njia ya mchakato wa marekebisho ya Katiba kufikia mwaka 2030. Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, amesema ushirikiano kupitia mazungumzo kati ya Serikali na viongozi wa dini umesaidia kutatua changamoto zinazohusu amani nchini.
Waziri Katambi ametoa wito wa kuendeleza mazungumzo hayo, akitahadharisha dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya dini yanayoweza kuleta mgawanyiko miongoni mwa wananchi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Mongoso Wambura, amesema lengo la mkutano huo ni "kuweka mikakati inayotekelezeka na mfumo wa uwajibikaji unaopimika" ili Jeshi liweze kutathmini utendaji wake mwaka hadi mwaka.
Mkutano huo umewakutanisha makamanda wa polisi wa mikoa, viongozi wa vikosi na maafisa waandamizi kwa lengo la kutathmini hali ya usalama nchini na kukubaliana kuhusu vipaumbele vya Jeshi kwa mwaka unaofuata.
.jpeg)





Post a Comment