TANZANIA YATOA WITO KWA MATAIFA YA BAHARI YA HINDI KUUNGANISHA NGUVU KULINDA UTAJIRI WA DOLA BILIONI 300




Tanzania imetoa wito kwa Mataifa ya ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kimazingira katika kulinda rasilimali za bahari zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 za Marekani, ikionya kuwa mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu yanatishia mustakabali wa uchumi wa buluu na maisha ya mamilioni ya wananchi wanaotegemea bahari kwa chakula na kipato.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais katika ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 

Akisisitiza umuhimu wa kutafsiri makubaliano ya kimazingira kuwa hatua madhubuti za kisera, kisheria na kibajeti, amezitaka nchi wanachama kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa buluu unaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na mgawanyo wa haki wa manufaa yake.

Akieleza umuhimu wa kiuchumi, Makamu wa Rais amebainisha kuwa ukanda huo unazalisha takribani dola bilioni 20.8 kila mwaka, huku huduma za mifumo ya ikolojia zikiwa na thamani ya dola bilioni 25 kwa mwaka na utalii ukichangia zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji huo. 

Zaidi ya watu milioni 65 wanategemea bahari moja kwa moja kwa maisha yao, wakati asilimia 90 ya biashara ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupitia bandarini, hali inayofanya bahari kuwa mhimili muhimu wa biashara, ajira, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo, utajiri huo unakabiliwa na tishio kubwa la mabadiliko ya tabianchi, ambapo joto la uso wa bahari linaongezeka kwa wastani wa nyuzi joto 0.1 kila muongo na kuchangia kupauka kwa matumbawe, kupanda kwa kina cha bahari na mmomonyoko wa pwani. 

Ukanda huo unahifadhi zaidi ya asilimia 30 ya mifumo muhimu ya matumbawe, mikoko na nyasi bahari duniani, huku mifumo ya ikolojia inayohifadhi kaboni ya buluu ikikadiriwa kuwa na tani milioni 400 za kaboni. Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi ndiyo tishio kubwa zaidi, hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe kujenga ustahimilivu na kulinda mifumo ya ikolojia.

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imeweka uchumi wa buluu na uhifadhi kuwa msingi wa mageuzi ya kiuchumi kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Sera ya Zanzibar ya mwaka 2020. 

Kupitia ukanda wa pwani wa kilomita 1,424, eneo la bahari ya mipaka la kilomita za mraba 64,000 na Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wenye kilomita za mraba 223,000, Tanzania inaendelea kuimarisha hifadhi za bahari, kupambana na uvuvi haramu, kukuza ufugaji wa viumbe vya majini, utalii endelevu na biashara ya kaboni, ikiwemo mradi wa TASFAM wenye thamani ya dola milioni 41 Zanzibar unaonufaisha wananchi 160,000.









Katika mustakabali wa Mkataba wa Nairobi, Makamu wa Rais ameainisha vipaumbele sita vya kikanda vinavyojumuisha utekelezaji wa sheria na bajeti, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kurejesha mikoko na matumbawe, kudhibiti uchafuzi wa plastiki na kemikali, kulinda bioanuai ili kufikia lengo la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya bahari ifikapo 2030, kuwekeza katika tafiti za kisayansi na teknolojia, pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, wanawake na vijana kupitia majukwaa mapya yaliyoanzishwa kwenye mkutano huo wa COP12.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Bi. Elizabeth Maruma Mrema, amepongeza miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi kwa kuweka msingi imara wa ushirikiano wa kikanda, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati baina ya serikali, taasisi za kisayansi, asasi za kiraia na sekta ya fedha ili kukidhi mahitaji ya kuendeleza uchumi endelevu wa buluu. 

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, ameeleza kuwa mkutano huo unatoa fursa kubwa ya kubadilishana maarifa na uzoefu kwa washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi 10 wanachama zikiwemo Tanzania, Kenya, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Madagascar, Mauritius, Shelisheli, Comoro na Ufaransa, ambao wamekutana kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026 chini ya kaulimbiu ya uchumi endelevu wa buluu kwa manufaa ya watu na mazingira.

No comments