TANZANIA, UNDP KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA AJIRA KWA VIJANA NA UWEKEZAJI



Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) katika kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana, kuendeleza elimu, kuvutia uwekezaji na kukuza sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la UNDP Duniani ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ubelgiji, Bw. Alexander De Croo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, jijini Bangkok, nchini Thailand.

Amesema ajira kwa vijana ni moja ya vipaumbele muhimu vya maendeleo ya Tanzania kutokana na muundo wa idadi ya watu nchini, ambao unaonesha kuwa sehemu kubwa ya wananchi ni vijana, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha kupata ujuzi, mitaji, teknolojia na masoko yatakayowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

Alisisitiza kuwa idadi kubwa ya vijana inaweza kuwa fursa muhimu ya kukuza uchumi iwapo itawezeshwa ipasavyo, lakini ikikosa fursa za kiuchumi inaweza kusababisha changamoto za kijamii na kiuchumi, hususan pale vijana wanapokosa matumaini ya maisha bora.

“Masuala ya ajira na vijana ni mapana sana. Tunahitaji kuhakikisha vijana wanapata ujuzi sahihi, mitaji nafuu ya kuanzisha biashara, teknolojia, maarifa na upatikanaji wa masoko ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya nchi,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu na miundombinu ya elimu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu, huku akibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupanua usawa wa upatikanaji wa elimu kwa wavulana na wasichana katika ngazi mbalimbali.

Hata hivyo, alisema ukuaji wa idadi ya watu unaendelea kuongeza mahitaji ya shule, walimu, vitabu na miundombinu mingine, hivyo uwekezaji endelevu unahitajika ili kuimarisha upatikanaji wa elimu na kuboresha ubora wake.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutambua fursa za uwekezaji na kuandaa miradi inayoweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, akieleza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa inaendelea na zoezi la kubaini fursa za biashara na uwekezaji katika Ushoroba wa Kati (Central Corridor), unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya ndani ya nchi kupitia miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo reli ya kisasa (SGR), huku kukiwa na uwezekano wa kupanua fursa hizo hadi nchini Rwanda.

“ukanda huu una fursa kubwa katika sekta za kilimo, madini, utalii, usafirishaji na uendelezaji wa vituo vya usafirishaji na ugavi wa bidhaa (logistics centres), zinazoweza kuvutia uwekezaji na kuchochea uzalishaji pamoja na ajira” alisema Mhe. Balozi Omar

Pamoja na hayo alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kupitia mapendekezo ya kamati zilizoundwa kuchunguza changamoto zinazokabili mfumo wa kodi na mazingira ya ufanyaji biashara ili kuboresha mfumo huo na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkiu wa Shirika la Maendelo la Umoja wa Mataifa - UNDP, Bw. Alexander De Croo, alieleza utayari wa Shirika hilo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza ajenda za maendeleo ya nchi, ikiwemo kuwawezesha vijana, kuimarisha ujuzi na kukuza fursa za kiuchumi kupitia ushirikiano na Serikali, sekta binafsi na taasisi nyingine za maendeleo.

Alisema uwekezaji unapaswa kuangaliwa kama mkakati wa muda mrefu wa maendeleo, hususan katika matumizi bora ya rasilimali za asili, ikiwemo madini adimu yanayohitajika katika mabadiliko ya mifumo ya nishati duniani. 

Bw. De Croo alitoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania kwa kuandaa Mifumo Jumuishi ya Kitaifa ya Ufadhili wa Maendeleo (INFFs), itakayosaidia kuimarisha upatikanaji na uratibu wa rasilimali za kugharamia vipaumbele vya maendeleo.

Alisema UNDP, kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji na Ukuaji wa Tanzania, inalenga kubadilisha fursa hizo kuwa miradi yenye nyaraka na mipango madhubuti ya kifedha na kibiashara inayoweza kuvutia wawekezaji, kabla ya Mkutano wa uwekezaji unaotarajiwa kufanyika Juni 2027 nchini Tanzania.

“Tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika maandalizi ya mkutano huo na kutafuta ufadhili wa miradi ya miundombinu endelevu na uchumi wa buluu kupitia ushirikiano na Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi na kuongeza mchango wa uwekezaji katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi” alisema Bw. De Croo

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Enock Koola na Maafisa wengine wa Serikali na UNDP.


MWISHO

No comments