TANZANIA NA MAREKANI ZAIMARISHA UHUSIANO



*Mahusiano ya Miji Dada na viwanja vya ndege yang’ara

 

BALOZI wa Tanzania wa Washington, Marekani, Dkt. Elsie Kanza amesema mahusiano ya Tanzania na Marekani yamezidi kuimarika na kuibua fursa kwenye sekta mbalimbali kama vile uchukuzi, utalii na mahusiano ya miji dada.

 

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, Balozi Dkt. Elsie Kanza alisema Tanzania imeendelea kushirikiana na nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, usafiri, nishati, elimu na mafunzo.

 

“Julai mwaka huu, Tanzania na Marekani zilisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) ya miaka mitano katika sekta ya afya yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1,” alisema Balozi Kanza na kuongeza kuwa wapo katika hatua za mwisho za kuanzisha uhusiano baina ya viwanja vya ndege na bandari kati ya Tanzania na Marekani.

 

“Tupo katika hatua za mwisho za kuanzisha uhusiano baina ya viwanja vya ndege (sister airports) kati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hartsfield-Jackson Atlanta, ambao unaongoza kwa kuhudumia abiria wengi zaidi duniani. Pia, tunaendelea na mazungumzo na Bandari ya Philadelphia ili kuanzisha uhusiano na bandari ya Dar es Salaam,” alisema.

 

Takwimu za mwaka 2025 zinaonesha kuwa uwanja wa Hartsfield-Jackson Atlanta unahudumia abiria milioni 106.3 kwa mwaka hali inayouweka kuwa uwanja wenye wasafiri wengi duniani, ikifuatiwa na viwanja vya Dubai (UAE) na Tokyo (Japan). Wastani wa abiria kwa siku ni 291,000.

 

Akitoa ufafanuzi kuhusu uhusiano wa Miji Dada, Balozi Dkt. Kanza alisema dhana ya miji dada ni muhimu kwani miji husika hushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kibiashara, kijamii, kitamaduni na kiuchumi.

 

“Miji na majiji ya Tanzania na Marekani imeendelea kuanzisha uhusiano wa miji dada (sister cities) na hadi sasa majiji 10 ya Tanzania na Marekani yana uhusiano wa miji dada. Mara ya mwisho kuingia makubaliano hayo ni mwaka 2025, ambapo majiji ya Mwanza na Tulsa, Oklahoma na majiji ya Dar es Salaam na Dallas, Texas, yalianzisha uhusiano huo.”

 

“Kwa sasa, mazungumzo yanaendelea ili kuanzisha uhusiano wa miji dada kati ya Jiji la New Orleans, Louisiana na Jiji la Zanzibar; Mbeya na Omaha, Nebraska; Morogoro na Oregon; Dodoma na Phoenix, Arkansas; pamoja na Dar es Salaam na Philadelphia, Pennsylvania,” alisema.

 

Miji dada mingine ambayo tayari imepata washirika ni Arusha na Durham, North Carolina; Tanga na Toledo, Ohio; Moshi na DelRay Beach, Florida; Bagamoyo na Vallejo, Califonia; Arusha na Kansas City, Missouri; Tarime na Milwaukee, Wisconsin; na Dar Es Salaam na Lansing, Michigan.

 

Akielezea kuhusu ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Marekani, Balozi huyo alisema kwamba jitihada za ubalozi zinaendelea kuzaa matunda ambapo mwaka 2025, thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani ziliongezeka kwa asilimia 18, Tanzania ikiwa imerekodi ziada ya biashara (trade surplus) ya takribani dola za Marekani milioni 120 dhidi ya Marekani.

 

Alisema mwaka 2024, biashara kati ya Tanzania na Marekani ilifikia dola za Marekani bilioni 1.4 ambacho ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

 

Kuhusu ufanyaji biashara chini ya Mpango wa AGOA, Balozi Dkt. Kanza alisema programu hiyo iliyodumu kwa miaka 25 ambayo awali ilifikia ukomo Septemba 30, mwaka jana, hivi sasa imeongezewa muda hadi Desemba, 2028. “Programu hiyo inasaidia baadhi ya bidhaa za Tanzania kuuzwa hapa Marekani kwa bei ya ushindani. Asilimia 42.85 ya mauzo yote ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani kwa mwaka 2024, yalifanyika chini ya AGOA,” alisema.

 

Katika kuendelea kuvutia biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Marekani, Balozi huyo alisema wameendelea kuandaa makongamano ya biashara na uwekezaji pamoja na ziara za kibiashara (trade missions) baina ya nchi hizo. “Kwa mfano, Juni 2026 tulishirikiana na taasisi ya Virginia Economic Development Partnership (VEDP) kupeleka kampuni tisa za kibiashara nchini Tanzania ambazo zilitembelea Tanzania Bara na Zanzibar kuangalia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.”

 

“Kwa sasa, tunashirikiana na Jiji la Chicago, Illinois kupeleka ziara ya wafanyabiashara Tanzania ifikapo Desemba 2026, kwa ajili ya kuangalia fursa zilizopo na kuwahamasisha kuzichangamkia. Kwa mwaka 2027, tayari tumeanza kushirikiana na majimbo ya Arizona na Pennsylvania kuandaa ziara za kibiashara kwenda Tanzania,” alisema.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA

OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, OKTOBA 23, 2026.


--

No comments