SERIKALI MBIONI KUKAMILISHA BODI YA WAJIOLOJIA NCHINI KULINDA SEKTA YA MADINI



Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kisheria utakaowezesha kuundwa kwa Bodi ya Usajili na Udhibiti wa Wajiolojia nchini.

Hatua hiyo inalenga kusimamia maadili, kuweka viwango vya kitaaluma, na kuondoa vishoka pamoja na wataalamu wasio waaminifu wanaoipotezea fedha serikali na wawekezaji kwa kutoa taarifa zisizo sahihi za jiosayansi, huku lengo kuu likiwa ni kuchochea utekelezaji wa shughuli za madini kwa kuzingatia weledi.

Hayo yamebainishwa Oktoba 15, 2026 mjini Dodoma na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, wakati akiwasilisha taarifa ya Mpango wa kuwainua na kuwaendeleza wachimbaji wadogo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Waziri Mavunde ameeleza kuwa taratibu za ndani za serikali zinaendelea juu ya mapendekezo ya muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wajiosayansi kwa ajili ya hatua zake muhimu za kupitishwa.

Waziri Mavunde ameieleza Kamati hiyo kuwa bodi hiyo itakuwa na mamlaka kamili ya kuratibu taaluma hiyo, kusajili wataalamu wenye sifa, na kuhakikisha ripoti zote za utafiti zinazotolewa nchini zinabeba uwajibikaji wa kisheria. 

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa chombo hiki kunakuja kama tiba ya kilio cha muda mrefu cha Jumuiya ya Wanajiolojia Tanzania (TGS), ambapo kwa miaka mingi sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya watu wasio na sifa kufanya tafiti za miamba na madini, jambo linalosababisha wachimbaji wadogo na wawekezaji kupoteza mitaji mikubwa kwa kufanya uchimbaji wa kubahatisha kutokana na taarifa zisizo sahihi.

Akielezea kuhusu manufaa kwa wawekezaji na wachimbaji, Waziri Mavunde amefafanua kuwa ujio wa bodi hii unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo, kwani kupitia ripoti ya utafiti iliyoidhinishwa na bodi, mchimbaji atakuwa na fursa ya kuwasilisha taarifa hizo katika taasisi za fedha ili kupata mkopo au kwa mwekezaji wa nje ikiwa na muhuri rasmi wa mtaalamu anayetambulika na kuwajibika kisheria.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Simon Songe, ameeleza kuwa kamati hiyo imeamua kuweka suala hilo kama kipaumbele chake cha kwanza katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya madini ili kulinda taswira ya nchi, hususan kwa wawekezaji na wachimbaji wadogo ambao kwa sasa wana mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa. 

Sambamba na hilo, kamati imesisitiza ukamilishaji wa haraka wa bodi hiyo na kuipongeza Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake kwa kazi nzuri inayofanya katika usimamizi na utekelezaji wa vipaumbele vilivyopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

No comments