NDEJEMBI ATAKA VIJANA WASIWE WATAZAMAJI SEKTA YA GESI NA MAFUTA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameiagiza Wizara ya
Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa
mpango mkakati utakaowawezesha vijana na kampuni za Kitanzania kunufaika na
fursa za ajira, zabuni na uwekezaji katika miradi ya mafuta na gesi asilia
nchini.
Makamu wa Rais ametoa maagizo
hayo leo, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini wa leseni nne za
utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West
Songo Songo, Eyasi
- Wembere na Lindi- Mtwara, iliyofanyika katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema ni
muhimu kuhakikisha Watanzania, hususan vijana na wanawake, wanapewa kipaumbele
katika ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni, huku kampuni za ndani zikiwezeshwa
kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha, ameitaka Wizara ya
Nishati kuimarisha mifumo ya tathmini, ufuatiliaji na usimamizi wa leseni hizo,
sambamba na kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, uwajibikaji
na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha na mgao wa faida.
Ameielekeza TPDC kushirikiana
na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, ujuzi na teknolojia ili kuongeza tija
katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, huku
akiwataka wadau kutanguliza uzalendo kwa Tafa, uadilifu, uchapa kazi
na maslahi ya Taifa
mbele.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea
kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, yanayozingatia uwazi, kutabirika kwa
mifumo ya kisheria, ushindani wa haki na ulinzi wa maslahi ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema,
pamoja na lengo la kukuza pato la Taifa kufikia dola za Marekani trillioni 1
kama iliyoainishwa kwenye dira ya Taifa ya 2050. Matarajio mengine ya leseni
hizo katika ugunduzi wa mafuta na gesi asilia ni ongezeko la mapato ya Serikali
kupitia mrabaha, kodi na mgao wa faida.
Amesema uzalishaji wa
umeme kwa kutumia gesi unatarajiwa kuchangia uzalishaji wa Megawati 70,000
(zitakazohitajika ifikapo 2050), na kukuza ujuzi, teknolojia, kuongeza ajira na
kupanua fursa kwa kampuni za Tanzania zinazotoa huduma katika sekta hiyo.
Ametaka uwepo wa usimamizi
madhubuti, nidhamu ya matumizi ya fedha na uwajibikaji. Ametoa rai kwa taasisi
zote zinazohusika na uwekezaji huu kuhakikisha Watanzania, hususan wanawake na
vijana wanapewa fursa za ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni. Vilevile, ni
muhimu kuimarisha ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani
wa mafuta na gesi.
Makamu wa Rais amesema lengo
la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuanzisha Kituo cha umahiri cha kuendeleza
ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi asilia ili kujenga
rasilimali-watu yenye ujuzi na itakayowezesha kuleta ustawi wa Uchumi jumuishi
na endelevu.
Awali, Waziri wa Nishati, Dkt.
Juma Zuberi Homera, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza
uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya nishati, akisema hatua ya TPDC
kukabidhiwa leseni na kumiliki vitalu vyake ni mafanikio makubwa katika
kuimarisha uwezo wa Taifa wa kutafuta na kuendeleza rasilimali za mafuta na
gesi.
Amesema dhamira ya Serikali ni
kuhakikisha gesi asilia inayoendelezwa inatumika katika shughuli mbalimbali,
zikiwemo matumizi ya majumbani, usafiri, uzalishaji wa umeme na viwandani, huku
wananchi na kampuni za ndani zikinufaika na uwekezaji huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, Mhandisi
Mussa Makame, amesema vitalu vinne vilivyohusika katika utiaji saini
viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ukusanyaji wa taarifa za
mitetemo kwa ajili ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Amesema shirika hilo litahakikisha
wananchi wanashirikishwa kikamilifu, kampuni za ndani zinapewa kipaumbele
kulingana na uwezo na utaalamu wao, pamoja na kutekeleza miradi ya uwajibikaji
kwa jamii (CSR) ili uwekezaji huo uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Imetolewa
na:
Ofisi
ya Makamu wa Rais,
Dar es
Salaam,
28
September 2026


Post a Comment