SPIKA ZUNGU: WASHIRIKI ZAIDI YA 2000 WAHAKIKISHA USHIRIKI WA MKUTANO WA 153 WA IPU ARUSHA
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, amesema hadi sasa washiriki zaidi ya 2000 kutoka nchi 149 wameshajisajili na kuthibitisha kushiriki katika Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), huku washiriki 147 wakiwa ni kutoka Tanzania.
Aidha amesema maandalizi yote yamkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha yamekamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 2, 2026, Mheshimiwa Zungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha mkutano huo kufanyika nchini, huku akiwataka wakazi wa Arusha kuonyesha ukarimu wao wa asili ili wageni wajionee uzuri wa Watanzania na kutumia fursa hiyo ya kipekee kukuza biashara na utalii ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kuutangaza mkutano huo tangu hatua za awali za maandalizi, akisisitiza kuwa sekta ya utalii kwa sasa inachangia asilimia 26 ya pato la serikali huku lengo likiwa ni kufikisha asilimia 45 na kuendelea kupitia ukarimu, upendo na mapokezi mazuri kwa wageni.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yaliyopo Geneva, Uswisi, Balozi Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi, amesema Tanzania ni moja kati ya nchi chache za Afrika zilizopata bahati ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa, sifa ambazo zimemwendea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali nchi kuwa mwenyeji na Bunge kwa uratibu wake.
Balozi Possi amesisitiza kuwa mafanikio ya mkutano huu yanatumika kama kipimo cha utayari wa nchi katika kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa ya siku za usoni, akitoa wito kwa wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wageni wote wanaondoka nchini wakiwa na taswira chanya na kumbukumbu nzuri kuhusu Tanzania.

Post a Comment