Mawaziri MOESNA wapongeza maboresho Bandari Dar
Mawaziri na makatibu wakuu kutoka nchi za Afrika Mashariki, Kaskazini na Kusini (MOESNA) wameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) kwa maboresho ya miundombinu na kuimarika kwa ufanisi wa shughuli za upakuaji na upakiaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, hatua inayochangia kurahisisha biashara katika ukanda huo.
Akiongea kwa niaba ya ujumbe huo, Katibu Mtendaji wa MOESNA, Bw. Kassim Mpaata, alisema ujumbe huo umeridhishwa na maendeleo na kasi ya maboresho yanayoendelea bandarini hapo, akiahidi kuendelea kuunga mkono matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam.
“Sisi Waganda tumekuwa tukitumia bandari hii kwa muda mrefu, lakini kwa sasa tumeshuhudia mabadiliko makubwa na kasi ya juu ya maboresho yanayofanyika hapa,” alisema Mpaata.
Bw Mpaata alisema kuwa mara zote wamekuwa wakihimiza nchi wanachama kuboresha miundimbinu yote ya usafirishaji hususani barabara, bandari na mipakani ili kufanya mazingira ya biashara kuwa rafiki kwa kila nchi mwanachama.
“Kwa mara nyingine tunaipongeza mamlaka hii kwa maboresho haya yote na kuwaomba kuyafanyia kazi changamoto ambazo zinabainishwa na wajumbe ili kuongeza utendaji kazi na ufanisi n akuendelea kuvutia wateja Zaidi”, alisisitiza Bw Mpaata.
Alisema maboresho hayo yanaimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bandari, kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.
Akiongea katika ziara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Abdallah Mitawi, alisema ziara ya ujumbe huo ililenga kujionea maendeleo ya miundombinu na kutathmini utendaji wa bandari hiyo.
“Tulipokea ujumbe wa mawaziri na makatibu wakuu 22 waliokuja kushiriki mkutano wa wanachama. Tulijadili masuala mbalimbali ya kiuchumi, na wakaomba kutembelea bandari yetu ili kujionea wenyewe utendaji wake,” alisema Mitawi.
Alisema ujumbe huo uliridhishwa na maboresho yaliyofanyika na kuahidi kuendelea kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara katika nchi zao kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuingiza na kusafirisha bidhaa, ikiwemo mazao ya kilimo na madini, kwenda katika masoko mbalimbali, hususan ya Mashariki ya Mbali.
Katika ziara hiyo, wajumbe walitembelea gati namba sifuri hadi saba. Katika gati namba sifuri, walishuhudia meli kubwa ikipakua magari, huku katika magati mengine wakiona meli za makasha zikiendelea na shughuli za upakuaji wa mizigo.
Mitawi alisema wajumbe hao walipata fursa ya kushuhudia meli kubwa iliyowasili moja kwa moja kutoka Japan ikiwa na uwezo wa kubeba magari 5,272, ikiwa ni rekodi mpya katika bandari hiyo.
“Leo tumepata bahati ya kuishuhudia meli kubwa kama hii kutoka moja kwa moja nchini Japan, yenye urefu wa mita 199.8 na iliyoweka rekodi katika bandari hii kwa kubeba magari 5,272,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Meli wa TPA, Nahodha Peter John, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bw. Plasduce Mbossa, alisema wajumbe hao walifurahishwa na mpangilio mzuri wa shughuli na ufanisi walioishuhudia bandarini hapo.
Alisema miongoni mwa maboresho makubwa yaliyofanyika ni kuongeza kina cha maji bandarini kutoka mita 12 hadi mita 14.5, hatua iliyowezesha bandari hiyo kupokea meli kubwa zaidi.
Aliongeza kuwa kina cha njia ya kuingilia meli na miundombinu mingine ya uongozaji wa meli vimeboreshwa, hivyo kuwezesha meli kubwa kuingia na kugeuka kwa urahisi zaidi.
Kwa mujibu wa Nahodha John, maboresho hayo yameongeza uwezo wa bandari kupokea meli zenye urefu wa hadi mita 305, ikilinganishwa na mita 234 hapo awali, huku kina cha maji kikiwa mita 14.
Aidha, alisema kiwango cha shehena inayohudumiwa na bandari hiyo kimeongezeka kutoka tani milioni 33.4 katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi tani milioni 33.7 katika mwaka wa fedha 2025/2026, jambo linaloashiria kuendelea kuimarika kwa shughuli za kibiashara.
Post a Comment