Likizo ya mwaka mzima 'Keko' kama ukiendekeza tabia za kijinga
Kama ulikuwa na tabia ya kutembea mtaani katika halmashauri ya Jiji maeneo ya Ilala huku umeuma sigara na kuivuta taratibu, halafu mwisho wa unaisigina kwa kisigino au unaitupa tu na pengine kukisukumia kishungi ndani ya mfereji au chemba ya maji machafu, basi ni muda wa kusimama kidogo,kutafakari na kuanza upya maisha yako.
Sheria ndogondogo za Halmashauri ya Jiji Manispaa ya Ilala zimeweka wazi orodha ndefu ya makosa ya kijingajinga ambayo wengi wetu tuliyachukulia kama sehemu ya maisha ya kila siku ya mjini. Lakini safari hii mchezo umebadilika: ukikutwa na kosa lolote kati ya hayo, kiwango cha chini cha faini ni shilingi laki tatu (Tsh 300,000/=), na kiwango cha juu kinaweza kufika hadi shilingi milioni moja (Tsh 1,000,000/=) hapo kwa hapo, au kifungo cha mwaka mmoja jela, au hata kupewa vyote viwili kwa pamoja—yaani unapigwa faini ya milioni na bado unaenda kuisoma namba jela kwa mwaka mzima.
Fikiria kwa mfano umeamka asubuhi na hamu yako ya sigara. Unaiwasha kwa mbwembwe, unaivuta, kisha unaamua kuitupa ovyo barabarani. Kibao hicho pekee kinakugharimu laki tatu au milioni moja papo hapo. Nusu ya moshi uliovuta inageuka kuwa msiba wa mkoba wako, ambapo fedha uliyopanga kununulia mfuko wa unga au kulipia kodi inatoweka kwa sekunde moja tu ya uzembe.
Orodha hiyo imesheheni tabia zetu zile za "kizushi" ambazo tulizoea kuzifanya bila hata kufikiria. Utakuta mtu anatembea barabarani ghafla anaamua kutema mate ovyo, mwingine anashindwa kuvumilia anajisaidia haja ndogo au kubwa sehemu isiyoruhusiwa, au anapiga matusi ovyo mtaani.
Wengine nao ni wataalamu wa kupiga picha kila mahali bila ruhusa, au kupiga rangi majumba na mabango ovyo bila kibali. Vyote hivyo vimo kwenye orodha ya dhambi zinazokuletea faini ya laki tatu hadi milioni moja au jela.
Hali kadhalika kwa wafanyabiashara na madereva, mazoea ya kupaki gari au kutengeneza pikipiki sehemu isiyoruhusiwa, kumwaga mafuta au maji machafu barabarani, kutoweka dastibini dukani, au kufungua baa na grosali nje ya muda uliopangwa, sasa ni njia ya mkato ya kuikamilisha milioni moja au kwenda likizo ya mwaka mmoja gerezani.
Wakati mwingine tuliona kutupa mfuko wa plastiki au kutoifunika mchanga na simenti kwenye gari ni mambo madogo yasiyo na kazi, lakini Halmashauri imetuma ujumbe mzito kwamba mtaani hakuna tena nafasi ya ushamba au uzembe wa kijinga. Ukiamua kuchezea sheria hizi, jiandae ama kufungua mfuko utoe milioni, ama kukusanya nguo zako uende ukaishi jela kwa mwaka mzima, au ukumbane na vyote viwili kwa mpigo.
Post a Comment