DKT. MWIGULU AINADI DIRA 2050 KWA WAWEKEZAJI WA UINGEREZA
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesemaTanzania inaingia katika safari mpya ya maendeleo ya miaka 25 ambapo DIRA 2050 imejipambanua na kutoa mwelekeo wa nchi inakotaka kwenda.
Amesema uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita ni kielelezo tosha cha mwelekeo huo huku akitaja miundombinu, nishati, maliasili na nguvukazi ya vijana kuwa baadhi ya vichocheo vya kuipeleka mbele nchi kiuchumi.
“Uwekezaji tunaofanya katika miundombinu na nishati unatupatia jukwaa thabiti la kunadi DIRA 2050. Maliasili zetu zinatoa fursa muhimu; idadi kubwa ya vijana ambao ni nguvukazi ni chachu zaidi na Bahari ya Hindi inatupa fursa ya kupata masoko mengi zaidi nje ya mipaka yetu,” alisema.
Dkt. Mwigulu aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 8, 2026) wakati akitoa hotuba kuu kwenye Kongamano la Uwekezaji Tanzania 2026 linalofanyika jijini London, Uingereza na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 kutoka maeneo mbalimbali.
“Kwa sasa tunachohitaji ni washirika walio tayari kuijenga nchi yetu pamoja nasi. Kwa hiyo, mwaliko wangu leo uko wazi kwenu, ninasema ‘Njooni Tanzania’ mtazame fursa zilizopo. Leteni mitaji, teknolojia, utaalamu na zaidi ya yote, tujenge ushirikiano wa muda mrefu,” alisisitiza.
Alisema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko tayari kushirikiana na wawekezaji walio makini na kufanya nao kazi ili kuweza kuzibadilisha fursa zenye matumaini kuwa uwekezaji wenye mafanikio. “Sura mpya ya mabadiliko ya kiuchumi ya Tanzania inaandikwa sasa. Ndiyo maana tunawaalika muwe sehemu ya mabadiliko haya,” alisema Waziri Mkuu.
Akifafanua kuhusu nguvu za kiuchumi ilizonazo Tanzania, Waziri Mkuu alisema: “Bado hatujaridhika. Tunajua wawekezaji hawawekezi kwa sababu tu uchumi wa nchi unakua bali wanawekeza wakati kuna hali ya uchumi inayotabirika.”
“Tunajua kwamba wanawekeza kwa sababu kuna miradi inayoweza kupata fedha kutoka kwenye mabenki, kanuni za uwekezaji ziko wazi, miundombinu inafanya kazi na Serikali iko tayari kusikiliza na kujibu vikwazo vinapotokea. Kwa hiyo, hii ndiyo njia tunayochukua tunapotekeleza DIRA 2050.”
Alisema DIRA 2050 kwa asilimia kubwa inasisitiza utendaji kazi unaojumuisha sekta binafsi kwani Serikali inatambua kwamba haiwezi kufanya kila kitu peke yake bila kuungwa mkono na sekta binafsi.
Katika kuchagiza uwekezaji nchini Tanzania, Waziri Mkuu aliwaeleza washiriki hao kwamba maeneo ambayo wanakaribishwa kufanya uwekezaji kuwa ni nishati, madini, kilimo na usindikaji wa mazao, ujenzi wa viwanda, miundombinu na usafirishaji, utalii na uchumi wa bluu, teknolojia na huduma za kifedha.
Mapema, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Balozi Mbelwa Kairuki aliwataka washiriki wa kongamano hilo waitumie vizuri fursa hiyo kwa kupata taarifa zaidi kuhusu uwekezaji unaoweza kufanyika nchini Tanzania na kuahidi kuwa milango ya ofisi yake itakuwa wazi ili kuhakikisha mahusiano yaliyozaliwa kutokana na kongamano hilo yanaendelea kuimarishwa.
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Dkt. Juma Malik Akil, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitilla Mkumbo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki.

Post a Comment