DAR ES SALAAM YALIPUKA KWA SHANGWE IKIMPOKEA MISS GRAND INTERNATIONAL JIHAN DIMACHK





Jiji la Dar es Salaam leo limegeuka kitovu cha furaha na heshima kubwa ya kitaifa kufuatia kurejea nchini kwa mrembo Jihan Mohin Dimachk, aliyeandika historia kwa kutwaa taji la dunia la Miss Grand International 2026 huko Thailand tarehe 10 Oktoba. 

Maelfu ya Watanzania, wakiwemo viongozi, wasanii mashuhuri, na wajumbe wa tasnia ya ulimbwende, wamejitokeza kwa wingi kumpokea shujaa huyo aliyepeperusha vyema bendera ya nchi na kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa.

Ndege iliyomrejesha mrembo huyo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kupokelewa kwa heshima ya juu ya 'water salute' kutoka kwa magari ya zimamoto ya uwanjani hapo. 

Mapokezi hayo yalihusisha msafara mkubwa uliomtoa uwanjani hapo kupitia maeneo mbalimbali ya jiji ikiwemo Kijitonyama, Darajani Tanzanite hadi Dar Village, huku akiwa anasindikizwa na msafara farasi wa Jeshi la Polisi na maelfu ya wananchi waliomshangilia kwa furaha kando ya barabara.

Akizungumza mara baada ya kutua nchini, Jihan amewashukuru Watanzania kwa kujitokeza kumpigia kura kwa wingi na kusema kuwa ushirikiano na mapenzi makubwa aliyopata kutoka nyumbani ndivyo vilivyompa ujasiri na nguvu ya kushinda taji hilo la dunia. 

Furaha hiyo iliongezeka zaidi pale alipokutana na wafuasi wake pamoja na wadau mbalimbali, akiwemo mfanyabiashara Niffer aliyefika uwanjani hapo na kubadilishana naye maneno ya baraka na shukrani.

Mapokezi hayo yamekusanya pamoja warembo mbalimbali wenye mataji nchini, akiwemo Miss Universe Tanzania 2026, Elizabeth Makune, na Miss Cham 2026, Sandra Giovinazzo, waliotaja ushindi huo kuwa ni hamasa kubwa na mwanzo wa enzi mpya katika ulimbwende. 

Naye aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2020, Rose Manfere, amebainisha kuwa mwitikio huu mkubwa unaonyesha jinsi jamii ya Kitanzania ilivyobadilika na kuanza kuithamini sekta ya ulimbwende kama fursa rasmi ya ajira na ajenda ya kukuza heshima ya nchi na maadili.

Sauti za sekta ya sanaa na burudani pia zilisikika kupitia msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny, aliyeeleza kuwa ushindi wa Jihan umeipa Tanzania heshima kubwa na kuonyesha mfano wa kuigwa wa umoja wa Watanzania unavyoweza kuleta matokeo makubwa duniani. 

Ushindi huu unaelezwa na wengi kuwa si tu mafanikio binafsi ya Jihan Dimachk, bali ni chachu ya kutangaza utalii wa Tanzania na kufungua milango ya fursa mpya kwa mabinti wa Kitanzania katika nyanja za kimataifa.

No comments