Serikali Yasisitiza Sheria za Habari, Yaonya Kuhusu Mtafaruku wa Taarifa Kidijitali




Serikali imesema inaendelea kurekebisha sheria mbalimbali za habari ili kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa taarifa sahihi na za uhakika ili wananchi waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuw ana taarifa mbalimbali zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi yanayowagusa wao na jamii ya Kitanzania.

Aidha serikali imesisitiza umuhimu wa kudumisha uadilifu katika kupeana taarifa ili kukabiliana na changamoto ya mtafaruku wa taarifa unaosababishwa na zama za kidijitali. 

Kauli imetolewa na Msajili wa Magazeti, Wakili Msomi Evordy Kyando, wakati akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO  kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa kwa Wote (IDUAI) 2026 iliyoambatana na mijadala mbalimbali katika hoteli ya Protea Dar es salaam.

Wakili  Kyando alikukumbusha kuwa haki ya kupata taarifa ni ya kila Mtanzania chini ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambapo upatikanaji wake unajumuisha wajibu wa taasisi za umma kutoa taarifa sahihi hata kabla hazijaombwa ili kuondoa upotoshaji wa aina zote ukiwemo wa taarifa za uongo (misinformation na disinformation) au taarifa za kweli zinazowasilishwa kwa lengo la kusababisha madhara (mal-information). 

Hata hivyo alisema kwamba jukumu la kusimamia uadilifu katika mnyororo wa taarifa sio la Serikali pekee, bali linahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa waandishi wa habari, asasi za kiraia, taasisi za elimu, watafiti na wananchi wote katika kujiridhisha na vyanzo na usahihi wa taarifa kabla ya kuzisambaza. 





Alisema katika mazingira ya sasa ambapo intaneti, mitandao ya kijamii, simu janja na teknolojia ya akili unde zinasambaza taarifa kwa kasi kubwa, ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za kuaminika zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kimaendeleo. 

Alisisitiza  kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Kudumisha Uadilifu katika kupeana Taarifa wakati huu wa Zama za Kidijitali: Mchango wa Hali ya Upatikanaji wa Taarifa katika Kukabiliana na Mtafaruku wa Taarifa” inatoa fursa ya kipekee ya kutathmini kama taarifa zinazotolewa zinakidhi vigezo vya ubora, usahihi, kuaminika, na uhalisia bila kumdanganya au kumpotosha mtumiaji. 

Pamoja na hayo Wakili Kyando alisisitiza msimamo wa Serikali na wajibu wa pamoja, Msajili huyo wa Magazeti alieleza kuwa jukumu la Serikali sio kutoa taarifa pekee bali ni kusimamia taasisi zake ili zitoe taarifa sahihi, zinazoeleweka na zinazofika kwa wakati kupitia njia zinazofaa, huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa rasmi kwa wakati huziba ombwe linaloweza kujazwa na uvumi.

Pia  Wakili Kiyando katika salamu zake alipongeza Coalition on Right to Information (CoRI) na Jamii Africa kwa kuandaa jukwaa  muhimu linalowaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, Asasi za Kiraia, vyombo vya habari na wanazuoni kutathmini masuala ya uhuru wa habari. 


No comments