Mrithi wa Ndejembi apatikana, Kadogosa Ujenzi, Ulega Katiba
RAIS Dk Samia Suluhu Hassan, amemteua Masanja Kadogosa kuwa Waziri wa Ujenzi katika mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri ambayo yanaonekana kulenga kuziba nafasi ya Deogratius Ndejembi ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais.
Aidha katika uteuzi huo Dk Juma Homera anakuwa Waziri wa Nishati, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Ndejembi kabla ya uteuzi wa kuwa Makamu wa Rais..Kabla ya uteuzi huo, Dk Homera alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Moses Kusiluka, uteuzi huo pia umehusisha viongozi mbalimbali.
Taarifa ya Ikulu imeendelea kusema kwamba Abdallah Ulega ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kabla ya uteuzi huu Ulega alikuwa Waziri wa Ujenzi.
Pia Asha Khamis Abdulla ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha anayeshughulikia masuala ya usimamizi wa fedha, Profesa Bruno Sunguya ameteuliwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Jabiri Omari Makame ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC); na Dk Idrissa Muslim Hijja ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha taarifa hiyo inasema uapisho wa mawaziri, manaibu mawaziri na makatibu wakuu wateule utafanyika kwa tatehe itakayopangwa baadaye.

Post a Comment