KARIAKOO NI SMART AREA: DC MPOGOLO ATANGAZA VITA DHIDI YA UCHAFU




Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema eneo la Kariakoo linatambuliwa kama smart area hivyo linatakiwa kuwa na viwango vya juu vya usafi. 

Mpogolo ameyasema hayo leo Septemba 12/2026 mara baada ya kuhitimisha zoezi la usafi katika Kata ya Kariakoo lililowakutanisha viongozi, wadau wa mazingira na wananchi wa Jiji la Dar es salaam. 

Alisema kutokana na  ukweli huo kila mmoja analazimika kuwajibika kikamilifu katika masuala ya usafi na kulinda mazingira.

Agizo hilo limetolewa kufuatia maagizo thabiti yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,  wakati wa kuapisha viongozi ikulu ya Kizimkazi yanayotaka Jiji la Dar es Salaam kupambana dhidi ya uchafu.

"... ni uchafu mitaani ... miji yetu haipaswi kuwa michafu... lazima tummaintain usafi wa nchi yetu, tuondoe uchafu..." alisikika Rais Samia akisema kwamba  ataketi na viongozi wa Dar es salaam kuzungumzia hali hiyo.

" Mheshimiwa rais anatupenda wana dar ers salaam, anatupenda wana ilala kwa kutuambia ukweli na mtu akikuambia ukweli anakupenda.Wewe ukitoka nyumbani kwako unaye mkeo umevaa koti nyuma limepasuka, akatoka akuacha ujuwe huyo mkeo hakupendi . Ukitoka nyumbani upo na mumeo umevaa gauni bahati mbaya mdada amepasi ameunguza mumeo kaona kakaa kimya ujuwe huyo hakupendi...." alisema DC Mpogolo akitoa mfano huo kuelezea kwanini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyokuwa na mapenzi makubwa kwa wanaDar es salaam kwa kuwaambia kuhusu suala la uchafu.









Alisema  Dar es salaam itatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan na hawatamuangusha mkuu wa mkoa Albert Chalamila.

Mpogolo alifafanua kuwa eneo la Kariakoo ni kitovu kikuu cha biashara na linapaswa kuendana na hadhi ya maeneo mengine muhimu kama ilivyo katikati ya jiji au kando ya barabara kuu za Nyerere, Kawawa, na Morogoro, ambazo zinapitwa na wageni wengi wanaotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea mjini.

Akielezea zaidi kuhusu umuhimu wa usafi huo, Mpogolo aliwasihi wakazi wote wa Wilaya ya Ilala na Kariakoo kuendelea kupokea na kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na viongozi wao wa mkoa, akisisitiza kwamba usafi ni afya na ni wajibu usiokwepeka wa kila mtu. 

Aidha alitoa shukrani za pekee kwa wananchi, viongozi, na wadau wote waliojitokeza kwa wingi kushiriki kazi hiyo ya kizalendo, huku akiwahakikishia kuwa upande wa uongozi na wananchi wa Ilala hawatamwangusha Rais Samia na wako tayari kufanya kazi kwa bidii hadi kufikia malengo yaliyokusudiwa.

No comments