DKT. KIKWETE AWASILI TABORA KUKAGUA MIRADI YA JMKF YA ZAHANATI, HUDUMA ZA AFYA YA JAMI
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Muasisi wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili mkoani Tabora kwa ajili ya kuanza ziara yake ya siku nne kuanzia tarehe 12 hadi 15 Septemba 2026, inayolenga kukagua zahanati za kisasa zilizojengwa na taasisi hiyo .
Mradi huo wa ujenzi umefadhiliwa na S. C. Johnson & Son, Inc., kampuni ya kimataifa ya Marekani inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za usafi wa nyumbani pamoja na kemikali mbalimbali za matumizi ya kila siku,yenye makao yake makuu Racine, Wisconsin.
Kuwasili kwa kiongozi huyo kunakwenda sambamba na ukaguzi wa utekelezaji wa mradi wa Jamii Salama, unaojumuisha zahanati mbili zilizojengwa katika vijiji vya pembezoni vya Wilaya za Sikonge na Uyui zenye lengo la kutoa huduma za afya kwa zaidi ya wakazi 36,000 ambao kwa miaka mingi walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata matibabu.
Katika ziara hiyo inayofanyika kwa ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya, na uongozi wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Kikwete anaanza ratiba yake rasmi kuanzia kesho Septemba 13, 2026 kwa kukagua mradi wa kliniki tembezi wa Jamii Salama katika Kitongoji cha Ipembe, Kata ya Kiloli, kabla ya kuendelea na ukaguzi wa zahanati na nyumba mbili za watumishi zilizojengwa wilayani Sikonge.
Septemba 14, 2026, atatembelea Kijiji cha Gengesita, Kata ya Kizengi, Wilaya ya Uyui, ambako atajionea shughuli za kliniki tembezi na baadaye kukagua zahanati nyingine mpya na nyumba mbili za watumishi zilizokamilika kujengwa katika eneo hilo.
Mradi huo wa kimkakati ulioanza ujenzi wake tarehe 16 Juni 2025 na kukamilika mnamo Aprili 2026 unalenga kupunguza changamoto kubwa za kiutendaji na usafiri zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa Gengesita waliokuwa wakisafiri takribani kilomita 152 kutoka makao makuu ya halmashauri na wakazi wa Ipembe waliokuwa wakisafiri kilomita 199.
Zahanati hizo mpya, ambazo zilianza kutoa huduma rasmi tangu Juni 2026, zina miundombinu kamili ya afya ya msingi ikijumuisha idara ya wagonjwa wa nje, kliniki ya afya ya uzazi na mtoto, wodi ya wazazi, vyoo vya umma, vichomea taka vya kisasa na mashimo ya placenta yaliyojengwa na kampuni ya INCINICO KILOBA Limited, sambamba na makazi ya watumishi yatakayohakikisha upatikanaji wa wataalamu wa afya na wauguzi wa kudumu.
Akizungumzia mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa JMKF, Bi. Vanessa Anyoti, ameeleza kuwa zahanati hizo ni ishara ya matumaini na utu kwa familia ambazo kwa muda mrefu zimesota kwa kufuata matibabu mbali, akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za dhati za kuunga mkono maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha ustawi na usawa wa upatikanaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini na ya pembezoni nchini Tanzania.




Post a Comment