NDEJEMBI ATOA WITO WA AMANI , AAHIDI KUTUMIKIA TAIFA KWA UADILIFU




MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amewasihi Watanzania kulinda na kudumisha amani ya nchi ili kuiwezesha serikali na wananchi kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi. 

Ndejembi alitoa mwito huo akiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake binafsi, ambapo alikutana na jamaa zake wa ukoo wa upande wa mama yake, akisisitiza kuwa utulivu wa taifa ndio msingi mkuu wa ustawi wa kiuchumi na kijamii.

Katika salamu zake kwa wananchi, Makamu wa Rais aliwahimiza vijana kujikita katika shughuli za maendeleo na kufanya kazi kwa bidii kama njia ya kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza uchumi. 

Alieleza kuwa serikali inatambua vijana ni nguvukazi ya taifa na ndio maana inawashirikisha katika michakato mbalimbali ya maendeleo, huku akiahidi kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa kumsaidia Rais na kuwataka Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wao ili watimize matarajio ya wananchi.

Ndejembi alisisitiza umuhimu wa wananchi kumwombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ili atekeleze malengo yake ya kuleta maendeleo, akibainisha kuwa tangu aanze kufanya kazi naye amejionea ana dhamira ya dhati ya kulitumikia taifa.

 Aliongeza kuwa kuwaombea viongozi ni desturi njema inayosaidia kuimarisha utulivu wa kitaifa, umoja, na utawala wenye busara, akifananisha na jinsi vikundi vya kidini vinavyofanya maombezi maalumu ya kuwawezesha viongozi kutumikia kwa uadilifu.

Awali, akizungumza na wananchi wa Mbuyuni wilayani Moshi waliokusanyika kumkaribisha, Ndejembi aliahidi kuendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu, umakini, na kujituma. 

Ndejembi, aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Rais Agosti 26 na kuapishwa Agosti 29, mwaka huu, alizaliwa Julai 12, 1983 mjini Moshi, akiwa ni mtoto wa John Louis Pancras Ndejembi kutoka Dodoma na Amina Shariff Mudhari mwenyeji wa Kilimanjaro.

No comments