Maandalizi mbio za mbuzi yakamilika,Mbuzi 70 waingizwa kambini
Na Beda Msimbe , BSKY Media
Mbuzi sabini wameshaingia kambini rasmi kwa ajili ya maandalizi makali ya kuelekea tamasha kubwa la Mbio za Mbuzi litakalofanyika Septemba 19 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nne usiku katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es salaam.
Mbio hizo zimehamia viwanja hivyo kutoka katika eneo lililozoeleka la Viwanja vya Farasi, Oyster Bay ambavyo kwa sasa vinatengenezwa maalumu kwa ajili ya michuano ya AFCON.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10 katika hoteli ya Sea Cliff, Rais wa Rotary Club ya Oyster Bay, Paul Muhato, amefafanua kuwa maandalizi yote ya mbio hizo yamekamilika huku akikaribisha wananchi na makampuni mbalimbali kuchangamkia fursa ya kudhamini na kuwekeza katika tukio hili ambalo limekuwa mhimili mkubwa wa maendeleo ya jamii.
Aidha katika mkutano huo Muhato alitaja wadhamini mbalimbali 34 ambao wameitika akiwemo mdhamini mkuu Vodacom na Benki ya NMB.Wadhamini wengine ni pamoja na TOYOTA, PEPSI, TBL, BOWMANS, YARA, RED N WHITE na SGA Security , Pian wapo TIKE TIKA, PREMIER CARE, PIGABET, JC DECAUX, Bevco na Captivate Africa.
"Tunawakaribisha wapenda burudani na makampuni mbalimbali yanayotaka kudhamini tamasha hili kwani nafasi bado ipo" alisema Muhato.
Alisema tamasha la mwaka huu limelenga kuchangisha zaidi ya sh milioni 200 kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kusaidia elimu na afya .
Pia aliendelea kuhimiza wananchi taasisi na hata makampuni kukuza ushindani kwa kudhamini mbuzi waliopo kambini ambapo mmoja anadhaminiwa kwa shilingi laki saba ambapo mdhamini anashiriki moja kwa moja kwenye mbio hizo huku akipata zawadi ya tiketi nne za kuingia uwanjani, na mshindi wa mbio hizo ataondoka na kitita cha shilingi laki nne taslimu sambamba na zawadi nono kutoka kwa wadhamini.
Wananchi watakaofurika uwanjani hapo watajionea mambo makubwa yakiwemo zawadi za mtoko nadhifu, burudani mbalimbali ikiwamo mbio za farasi, na michezo ya bahati nasibu huku milango ikiwa wazi kwa viingilio vya shilingi 30,000 kwa watu wazima, elfu 10 kwa watoto, na shilingi laki mbili kwa viti maalum vya VIP.
Lengo kuu la kishindo hiki cha burudani ni kuhakikisha kuwa baada ya kuondoa gharama zote za uendeshaji, wabakize shilingi milioni mia mbili kamili ambazo zitakwenda moja kwa moja kutoa udhamini wa elimu kwa wanafunzi 150 wa mwaka 2027, ikiwa ni mwendelezo mzuri wa msimu uliopita ambapo walikusanya Shilingi milioni 167 zilizosaidia shughuli mbalimbali za jamii ikiwamo sekta za elimu na afya.
Tamasha hili lenye mizizi yake tangu mwaka 2001 lilipoanzishwa na kamati ya kujitolea ikiongozwa na Abdu Simba na Karen Stanley kwa mfumo ulioigwa kutoka Uganda na mashindano ya Royal Ascot ya Uingereza, liliokolewa na Rotary Club of Dar es Salaam Oyster Bay mwaka 2018 ili lisife, likithibitisha kwamba furaha ya leo ni mchango mkubwa wa kesho kwa jamii yetu.






Post a Comment