TMA Yataka Sekta Zijipange Kukabili Athari za El Niño



Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari, amezitaka sekta zote nchini kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa katika kupanga na kuchukua hatua za kukabiliana na athari zikazosababishwa na El Niño inayotarajiwa kuendelea kuimarika kuelekea mwishoni mwa mwaka 2026.

Alisema hayo, alipokuwa akifungua Mkutano wa 25 wa kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli za Oktoba hadi Desemba 2026 mjini Dodoma na kueleza kuwa ni muhimu wadau kufuatilia taarifa hizo mapema kutokana na nchi kuendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ongezeko la joto, ukame, upepo mkali, vimbunga na vipindi vya mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko. 

Alisema kuwa taarifa hizo zinapaswa kutumika katika kufanya maamuzi na kupanga shughuli badala ya kuonekana kama taarifa za kawaida pekee.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dk. Ladislaus Chang’a, aliongeza kuwa mamlaka hiyo imeendelea kuboresha utoaji wa taarifa kwa kuandaa utabiri mahususi kwa wilaya 86 za mikoa inayopata mvua za Vuli ili kukabiliana na changamoto hiyo ya El Niño inayochagiza mvua hizo. 

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Makame, alisisitiza kuwa utabiri huo wenye kaulimbiu “Kupunguza Pengo la Uelewa wa Tahadhari za Hali ya Hewa kwa Pamoja,” ni muhimu katika kuwawezesha jamii na sekta kujiandaa, kukabiliana na majanga na kurejesha hali baada ya maafa, huku mkutano huo ukiwasilisha pia mrejesho uliouonesha msimu wa mvua za Masika uliopita kuwa na kiwango cha usahihi cha asilimia 94.1.

No comments