WAZAZI WATAKIWA KUJENGA MAADILI KWA WATOTO


Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha watoto wanapata elimu inayojenga maadili, hofu ya Mungu na kukuza vipaji vyao ili kuwaandaa kuwa raia wema wenye mchango chanya katika jamii. 

Wito huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Mchungaji wa Makanisa ya Mlima wa Moto, Rose Mgeta katika maombi maalumu ya kuwaombea watoto na wanafunzi wa Tanzania yaliyowakutanisha wazazi, wanafunzi na jamii ya Shule za St Mary’s.

 Alisema maombi hayo ni sehemu ya utamaduni ulioasisiwa na mwanzilishi wa taasisi hizo, Askofu Getrude Rwakatare na unaoendelezwa na uongozi wa sasa kwa lengo la kuwaombea watoto, wazazi na taifa kwa ujumla, huku akiwahimiza wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto wao wenye umri wa kwenda shule kuhakikisha wanawapeleka kwani elimu ni msingi wa maisha.

Kwa upande wake, Meneja wa Shule za St Mary’s, Muta Rwakatare alisema taasisi hiyo imejipanga kutekeleza mtaala mpya unaoweka mkazo katika elimu ya ufundi, matumizi ya teknolojia za kidijiti na ukuzaji wa ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa. 

Alisema mbali na masomo ya darasani, shule hizo zimeendelea kuwekeza katika michezo, sanaa na shughuli mbalimbali za kukuza vipaji ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea na kushindana katika soko la ajira, huku akiomba serikali kuendelea kuziwezesha shule binafsi katika utekelezaji wa mtaala huo mpya hususan kupitia uimarishaji wa mazingira ya elimu ya kidijiti na sayansi.

No comments