Katambi: SMZ na Jamhuri Zaimarisha Mafunzo ya Amali Kukuza Ajira
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejipanga kuimarisha mafunzo katika vyuo vya amali ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaowawezesha kushindana katika soko la ajira na kujiajiri.
Alisema hayo, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali eneo la Kangagani Pemba na kuwataka wazazi kuwahamasisha vijana kujiunga na vyuo hivyo kupitia fursa za elimu ya ufundi na vitendo.
Alisema kuwa serikali zote mbili zimetambua umuhimu wa elimu ya amali kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana huku Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Jamhuri ya Muungano zikisistiza kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kushiriki katika shughuli za kiuchumi badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Salum Ali, aliyeeleza kuwa katika Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 wizara imepanga kujenga vyuo vitano vya mafunzo ya amali kupitia mradi wa Sebeb.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said, alieleza kuwa ujenzi wa vyuo hivyo umeanza kuleta mafanikio makubwa kwa kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta binafsi na kubadili mtazamo kwamba ajira zinapatikana serikalini pekee.

Post a Comment