TFF YAJA NA MFUMO MPYA UNUNUZI WA TIKETI


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeanza kutumia mfumo mpya wa ununuzi wa tiketi kuanzia mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba unaotarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja. 

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema mfumo huo ambao ni rahisi kuutumia unatoa fursa ya kununua tiketi nne kwa mtu mmoja na zitakuwa na majina. 

“Tiketi zinapatikana kidijiti pekee kupitia tovuti ya TFF Tickets. Tiketi zitakuwa na majina ya watumiaji kwa sababu za kiusalama na mtu mmoja anaruhusiwa kununua zisizozidi tiketi nne kwa kutumia namba moja ya simu,” alisema. 

Pia, Ndimbo alisema sababu za mchezo kupelekwa uwanja wa New Amaan Complex ni kwa sababu ndiyo uwanja pekee uliokuwa tayari na wenye vigezo kamili kwa sasa kuandaa mchezo huo mkubwa.

 Kuhusu masuala ya gharama na umbali kwa mashabiki alisema hayakwepeki kwani hata mchezo ungepelekwa mikoani kama Mwanza au Kigoma bado changamoto ya usafiri ingekuwepo kwa baadhi ya mashabiki. 

Mchezo wa Ngao ya Jamii ambao huwakutanisha Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Bingwa wa Kombe la Shirikisho, na unaashiria kufunguliwa rasmi kwa msimu mpya wa soka. 

Mapato yanayopatikana kwenye mchezo huo hutumiwa na TFF au wadhamini kufanya kazi za kijamii; kusaidia hospitali, vituo vya watoto yatima au kukuza soka la vijana. 

Yanga na Simba zinakutana kwenye mchezo huo ikiwa ni siku chache baada ya kucheza michezo wa kirafiki katika matamasha yao na zote kufungwa. 

No comments