DC MPOGOLO AAGIZA SULUHISHO LA KUDUMU CHANGAMOTO YA MAJITAKA BUGURUNI KISIWANI



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amezitaka kampuni za CRJE na TAISHAN kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam katika kutafuta na kutekeleza suluhisho la kudumu la changamoto ya maji na majitaka katika eneo la Kisiwani, Kata ya Buguruni, ikiwemo ujenzi wa mfereji maalumu wa majitaka.

Agizo hilo limetolewa baada ya DC Mpogolo kufika na kukagua eneo hilo kufuatia kilio cha wananchi wanaolalamikia kuzibwa kwa mifereji, ambapo amejionea hali halisi ya miundombinu na kubaini kuwa baadhi ya mifumo imeathiriwa na shughuli za ujenzi zinazoendelea, yakiwemo maeneo ambapo mfereji uliokuwa ukipitisha maji kuelekea Mto Msimbazi kuzibwa na kampuni  hizo kutokana nashughuli za ujenzi.

Katika ukaguzi huo, DC Mpogolo alitembelea maeneo yote ya mfereji na kubaini makosa mbalimbali ikiwemo baadhi ya kaya kutiririsha maji taka na maji ya vyoo moja kwa moja kwenye mfereji huo wa maji ya mvua, jambo linalofanya mfereji huo kuwa na maji wakati wote; aidha alibaini kuwepo kwa msikiti uliojengwa juu ya mfereji huo ambao unaweza kupata athari kubwa pindi mafuriko yatakapotokea. 

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa kuwahamasisha wananchi kuunganisha mifumo yao ya vyoo na miundombinu ya DAWASA badala ya kutiririsha maji taka ovyo, huku akibainisha kuwa tayari serikali imetoa fedha kwa ajili ya mfumo ila kiulichobaki ni kwa wananchi wenyewe kwenda dawasa kuelezea mahitaji ya kuunganishwa.

Alisema mfereji huo lazima uwe wazi kutokana na watu wa hali ya hewa kusema kwamba mvua za mwaka huu zitakuwa za elnino.

Ili kupata suluhu ya haraka, DC Mpogolo ametangaza kuwa Jumatatu wataalamu kutoka kampuni ya CRJE, TAISHAN ,TARURA na Halmashauri ya Jiji wafike katika eneo hilo na kutoa sulkuhusu litakalowezesha kujengwa kwa mfereji huo wa kusafirisha maji taka kuelekea mto Msimbazi.

Alisema mainjinia hao kwa pamoja wataangalia namna bora ya kusafirisha maji kuanzia ukanda huo mpaka Mto Msimbazi .

No comments