WADAU WA SIASA WAIUNGA MKONO TUME YA UCHUNGUZI YA RAIS SAMIA



Wachambuzi wa siasa nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, huku wakipendekeza matokeo yake yawe chachu ya kuleta maridhiano na uwajibikaji utakaokuwa fundisho kwa wengine. 

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini, Juma Ali Khatibu, alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza ushauri wa kuchunguza uvunjifu wa amani, akisema wajumbe walioteuliwa wakiwemo majaji wastaafu na wengine wawili kutoka nchi za Uganda na Namibia wana uwezo mkubwa wa kutenda haki. 

Alisisitiza kuwa tume hiyo ipewe nafasi na ushirikiano ili mkono wa sheria uwawajibishe wote waliochochea vurugu hizo ili iwe fundisho kwa siku za mbele.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, akizungumza na kituo cha televisheni cha UTV, alieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa pendekezo lao la awali na kueleza kuwa mwisho wa siku kazi ya tume hiyo inapaswa kulenga kuleta maridhiano kati ya pande zilizogombana ili kumaliza kabisa migogoro.

 Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Benson Kigaila, aliongeza kuwa baada ya kuundwa kwa tume hiyo, jukumu lililopo ni kusubiri, kushirikiana nayo na kuendelea na majadiliano zaidi mara baada ya kupokea taarifa rasmi ya uchunguzi huo.

No comments