MSIGWA: AFCON HAITAHAMA, TANZANIA TAYARI KUWA MWENYEJI

 



Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa nchi ipo tayari kuwa mwenyekiti mwenza wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2027, huku ikitupilia mbali hofu na dhana potofu zilizopo kwamba michuano hiyo inaweza kuhamishiwa nchi nyingine.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro, ambapo aliwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zinazodai kuwa Tanzania inaweza kupoteza nafasi hiyo ya uenyeji.

Msigwa alisisitiza kuwa michuano hiyo haitahama na kwamba maandalizi yote yanafanyika kwa kasi inayotakiwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania, Kenya na Uganda kama ilivyopangwa tangu awali.

Akielezea hatua za ujenzi na ukarabati wa miundombinu, alisema kuwa uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam upo katika hatua za mwisho, wakati Uwanja wa Samia Suluhu Hassan uliopo Arusha umefikia zaidi ya asilimia tisini na Uwanja wa Fumba uliopo Zanzibar umekamilika kwa zaidi ya asilimia sabini na tano.

Katika hatua nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali aliwakumbusha wananchi na wafanyabiashara kwamba michuano hiyo ya AFCON haipaswi kutazamwa kama tukio la michezo pekee, bali inapaswa kuchukuliwa kama fursa kubwa ya kiuchumi itakayochochea maendeleo katika sekta za utalii, kilimo, biashara na uwekezaji.

Alifafanua kuwa wageni na watalii watakaowasili nchini wakati wa michuano hiyo hawatabaki katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar pekee, bali watatembelea mikoa mingine na kujionea bidhaa za ndani, ikiwemo uzalishaji wa sukari na mchele mkoani Morogoro.

Hivyo, aliwataka wajasiriamali, wamiliki wa hoteli, wasanii, na wananchi kwa ujumla kujiandaa mapema kwa kutumia fursa hiyo kujenga mahusiano ya kibiashara na kutangaza utamaduni wa Tanzania kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali

No comments