KUGEUZA UBUNIFU KUWA MALI YENYE THAMANI: NINI KIFANYIKE BAADA YA MAONYESHO YA MASHARIKI CREATIVE ECONOMY EXPO 2026
Maonyesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026 yaliyohitimishwa hivi jana katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Culture and Development East Africa yameacha alama kubwa kwa wadau wa sekta ya ubunifu, sanaa na utamaduni hapa nchini na barani Afrika.
Tukio hili limewakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya BAKITA Profesa Martin Mhando, Mwenyekiti wa Bodi ya BASATA Profesa Saudin Mwakaje, Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Dkt. Mona Mwakalinga, Kaimu Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bi. Naomi Mungure, pamoja na wageni wa kimataifa kama mwanamuziki nguli Yvonne Chaka Chaka kutoka Afrika Kusini.
Kupitia mijadala, ziara za mabanda na uwasilishaji wa mada mbalimbali, imedhihirika wazi kuwa sekta ya ubunifu ina uwezo mkubwa wa kuchangia pato la taifa, lakini mafanikio haya hayapaswi kuishia kwenye makongamano na semina za siku chache tu.
Msisitizo uliotolewa na Profesa Saudin Mwakaje kuhusu umuhimu wa kuanzisha mfumo madhubuti wa kutathmini thamani ya kazi za ubunifu ili kumlinda mbunifu na kumwezesha kunufaika kiuchumi unapaswa kuwa ajenda ya kudumu na si maneno ya kwenye makaratasi.
Mara nyingi wasanii wetu wamekuwa wakipoteza haki miliki zao au kushindwa kunufaika kifedha kutokana na ukosefu wa mifumo thabiti ya kisheria na kibiashara inayotambua thamani halisi ya kazi zao.
Hivyo basi, wadau na taasisi husika kama BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zinapaswa kuchukua hatua za haraka za vitendo kwa kushirikiana na serikali ili kujenga mnyororo rasmi wa kiuchumi utakaomwezesha msanii kunasa mapato halisi ya kazi zake sokoni, badala ya kubaki na umiliki wa jina pekee bila faida za kifedha.
Aidha, ujio na nasaha zito zilizotolewa na mwanamuziki Yvonne Chaka Chaka kuhusu umuhimu wa elimu, maadili, ushirikiano na kurasimisha shughuli za sanaa zinatoa mwanga kuwa vijana wetu wanapaswa kubadilisha mtazamo na kuichukulia sanaa kama biashara inayohitaji weledi na mipango thabiti.
Ili maonyesho haya yawe na tija ya kudumu, haitoshi tu kukutana na kubadilishana mawazo wakati wa maonesho, bali kunahitajika mikakati ya ufuatiliaji wa karibu itakayowahusisha vijana wenyewe katika kujenga ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kama vile kufanya kazi za pamoja zitakazopanua wigo wa masoko ya muziki na filamu za Kitanzania nje ya mipaka ya nchi.
Kazi kubwa iliyoko mbele yetu sasa baada ya maonesho haya ni kuanzisha program za mafunzo endelevu za mara kwa mara huko mikoani na kwenye vituo vya vijana ili kutoa elimu ya haki miliki, ubunifu wenye tija, na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kama rasilimali ya kiuchumi.
Serikali kupitia wizara na taasisi zake inapaswa kuweka mazingira rafiki ya kifedha na kodi kwa wawekezaji katika sekta ya ubunifu ili kuvutia mitaji mikubwa itakayojenga viwanda vya filamu, muziki na ubunifu wa kidijitali nchini.
Ni wakati sasa wa kuacha kuona sanaa kama burudani ya kupitisha wakati na badala yake kuisimamia kama nguzo kuu ya uchumi wa buluu na ubunifu itakayowaondolea umaskini vijana na kuliingizia taifa tija inayostahili.

Post a Comment