Kamati ya saa 72 yatoa onyo Kanuni ya 20




KAMATI ya saa 72 imekumbusha timu zote kuzingatia kikamilifu Kanuni ya 20 inayohusu matumizi ya Msaada wa Video katika Soka (FVS) ikisisitiza kuwa mchezaji haruhusiwi kumlalamikia au kumshinikiza mwamuzi kuomba marejeo ya tukio. 

Kwa mujibu wa Kanuni ya 20 (4), kocha mkuu au kiongozi mwingine wa juu kwenye benchi la ufundi pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuwasilisha ombi la marejeo ya tukio katika mfumo wa FVS kupitia mwamuzi wa akiba. 

Kanuni hiyo pia inaelekeza kuwa iwapo mchezaji ataona tukio linahitaji marejeo ya FVS, anatakiwa kumjulisha kocha mkuu au kiongozi wa benchi la ufundi kwa ishara ili kiongozi huyo awasilishe ombi hilo. 

Katika taarifa iliyotolewa juzi na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), ilisema Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeonya kuwa ni marufuku kwa mchezaji kumkabili, kumlalamikia au kumshinikiza mwamuzi moja kwa moja kwa lengo la kuomba marejeo ya FVS. 

Mchezaji atakayekiuka masharti hayo ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17 inayohusu taratibu za mchezo, kipengele cha 62 ambacho kinasema: “TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wowote wa taratibu za mchezo kama zilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Shilingi milioni 10 na/ au kufungia michezo isiyozidi mitatu au kipindi kisichozidi miezi mitatu. 

“Faini kwa makosa yanayojirudia itatozwa kati ya Shilingi milioni 11 na Shilingi milioni 40 kwa mchezaji, kiongozi au klabu”. Kamati ilisema itaendelea kusimamia utekelezaji wa kanuni hizo na kuchukua hatua dhidi ya wachezaji au timu zitakazobainika kukiuka masharti yaliyowekwa.


No comments