IGP WAMBURA AWATAKA ASKARI KUZINGATIA UTU NA WELEDI
Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amewataka askari polisi
kuhakikisha huduma wanazotoa kwa wananchi zinazingatia utu, haki, weledi na
huruma, hususan wanaposhughulikia waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili
dhidi ya watoto.
Akizungumza
jana jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Watendaji wa Madawati ya Jinsia
na Watoto kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, sambamba na uzinduzi wa Kituo cha
Mawasiliano cha Gender-Based Violence and Violence Against Children na Kitabu
cha Mwanafunzi na Mwongozo wa Mwalimu wa Somo la Polisi Jamii, IGP Wambura
alisema mafanikio ya jeshi hilo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya mikutano au
mifumo inayozinduliwa, bali kwa idadi ya waathirika wanaopata msaada na kiwango
cha imani ambacho wananchi wanacho kwa jeshi hilo.
Alisisitiza
kuwa mafunzo na teknolojia lazima yatafsiriwe katika ubora wa huduma
inayozingatia haki na weledi, huku akibainisha kuwa watendaji wa madawati hayo
hukutana na watu waliopitia maumivu na hofu hivyo wanapaswa kutekeleza sheria
kwa busara na huruma kwani kulinda wanawake na watoto ni msingi wa amani na
maendeleo ya taifa.
Aidha,
alieleza kuwa vitabu vilivyozinduliwa vitasaidia kuimarisha mafunzo na weledi
wa askari, wakati Kituo cha Mawasiliano kitawawezesha wananchi kutoa taarifa
kwa haraka, kupata ushauri na kuelekezwa kwenye huduma stahiki, hatua
itakayoongeza ufanisi kwa manusura wa ukatili na kuimarisha uhusiano mzuri kati
ya Jeshi la Polisi na jamii.

Post a Comment