Dkt. Mwigulu atatua mgogoro wa ardhi Goba uliodumu miaka 28
Waziri Mkuu Dkt.
Mwigulu Nchemba leo Agosti 15, 2026
ameendelea kutatua kwa njia ya
maridhiano migogoro sugu inayowakabili
wananchi na mara hii ametatua mgogoro wa
ardhi kati ya Bi. Alia Shariff na Bi
Devotha Delfina Elisei uliodumu miaka 28 katika eneo la Goba jijini Dar es
salaam .
Bi. Alia Shariff,
mkazi wa Dar es Salaam, alimwandikia barua
Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 20 Januari 2026, akiomba amsaidie kutatua mgogoro huo na katika barua hiyo, alieleza kuwa eneo
analolalamikia limemilikiwa na
wanae tangu mwaka 1998 na kwa muda wote huo ametafuta suluhu ya jambo
hilo bila mafanikio.
Waziri Mkuu
alituma Timu ya Watalaam kutoka Ofisini kwake ikiongozwa na Mwenyekiti ambaye
pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Mahusiano, Asasi za Kiraia na Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali, Bw. Tryphone Mkolokoti, na Katibu wake ambaye pia ni Msaidizi wa
Waziri Mkuu – Masuala ya Ardhi, Bw. Senso Magessa ambayo ilishirikiana na Kamishina Msaidizi wa
Ardhi Mkoa wa Dar es salaam, Shukuruni Kyando, Watalaam wa Ardhi Manispaa ya
Kinondoni pamoja wa viongozi wa Kata na Mtaa wa Goba lilipo eneo lenye mgogoro.
Timu iliitisha
vikao vya usuluhishi na kutembelea eneo
la mgogoro vilivyowahusisha Watalaam wa masuala ya ardhi Mkoa wa Dar es salaam
na wilaya ya Kinondoni, majirani na wazee walioishi miaka mingi pamoja na wapima ardhi ambao walihakiki na
kubainisha mipaka halali ya viwanja Namba
202, 203, 204 na
205, vilivyopo Goba, jijini Dar es Salaam vilivyokuwa na mgogoro.
Baada ya
uchambuzi wa nyaraka, maelezo ya pande
mbili zilizohuka katika mgogoro huo na upimaji uliofanywa imebainika
kuwa uamuzi wa Mahakama umeelekeza kuwa
kiwanja Na. 202 chenye ukubwa wa
zaidi ya mita za mraba 3,000 ambapo Devota anamiliki mita za mraba 1,000
ndicho kiini cha mgogoro.
Pande zote mbili
zimekubaliana kuheshimu hukumu, amri na maamuzi halali ya Mahakama, pamoja na
kufuata taratibu zinazotakiwa na mamlaka za ardhi katika kubainisha na
kutekeleza haki za kila upande na kuepuka vitendo vinavyoweza kuibua mgogoro
tena.
Utiaji saini
nyaraka za maridhiano hayo ulifanyika kwenye eneo lililokuwa na mgogoro
Goba jijini dar es salaam na kushuhudiwa na
Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Dar es salaam, Shukuruni Kyando, Watalaam
wa Ardhi Manispaa ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es salaam, Watalaamu kutoka ofisi
ya Waziri Mkuu, Viongozi wa eneo la Goba na wananchi.
Kamishna wa Ardhi
Msaidizi Mkoa wa Dar es salam Shukuruni Kyando alitumia fursa hiyo kutoa elimu
ya namna sahihi na ya haraka ya kubatilisha hati miliki ya ardhi na kupata hati
mpya na halali katika maeneo yenye migogoro ambayo utatuzi wake ulisababisha kiwanja
hicho kugawanywa kwa mmiliki zaidi ya mmoja.

Post a Comment