Masauni atoa wito jamii kulinda udongo na mazingira


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesisitiza kuwa afya ya udongo ni nguzo kuu ya usalama wa chakula, uhifadhi wa mazingira, na ustawi wa uchumi wa taifa.

Aidha, kutokana na ukweli huo amemtaka kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuutunza. 

Wito huo aliutoa jijini Dar es Salaam wakati akishiriki katika matembezi ya kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira yaliyojulikana kama ‘Save Soil Walkathon’ yaliyofanyika Julai 19, 2026. 

Mhe. Masauni alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaweka kipaumbele kikubwa katika ajenda ya uendelevu wa mazingira kama sehemu ya mkakati wa maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa udongo ni rasilimali muhimu inayobeba maisha ya kila siku ya binadamu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Masauni alieleza kuwa bila udongo wenye afya hakuna usalama wa chakula wala mazingira bora kwa maendeleo endelevu, hivyo ni wajibu wa kila raia kutumia ardhi kwa njia rafiki ili kuhifadhi uhai wake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Waziri aliongeza kuwa utekelezaji wa mipango hii ya mazingira unafungua fursa nyingi za ushirikiano na Jamhuri ya India, hasa katika nyanja za uhamishaji wa teknolojia, utafiti, uvumbuzi, na ujenzi wa uwezo wa kitaalamu. Alibainisha kuwa ushirikiano huo unalenga kusaidia urejeshaji endelevu wa ardhi, ufuatiliaji wa mazingira, uwekezaji rafiki, pamoja na kupata suluhisho stahiki za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.





Kwa upande wake, Rais wa Lions Club of Dar es Salaam Mazingira, Bi. Lion Ramadevi, alieleza kuwa matembezi hayo ni sehemu ya kampeni pana inayolenga kuijengea jamii uelewa wa kina kuhusu mchango mkubwa wa udongo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Alisisitiza kuwa ‘Save Soil Walkathon’ si tukio la kawaida tu, bali ni harakati za kifikra zinazohamasisha mabadiliko ya tabia kwa wananchi, taasisi, na sekta binafsi ili kuchukua hatua za pamoja za kulinda mazingira kwa ajili ya mustakabali wa taifa. 

Naye Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Lakshay Anand, alipongeza jitihada hizo akieleza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona jamii ikitambua umuhimu wa kulinda mazingira, hatua ambayo ndiyo msingi mkuu wa kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu katika utunzaji wa viumbe hai na ustawi wa maisha ya binadamu kwa ujumla.

No comments