TFF Kufanya Mafunzo Maalumu ya Usalama na Ulinzi
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mpango wa kuendesha mafunzo ya usimamizi wa michezo kwa Maofisa Ulinzi na Usalama wa Michezo, yaliyopangwa kufanyika kuanzia Agosti 5 hadi 6, 2026, katika Kituo cha Ufundi cha TFF kilichopo Mnyanjani mkoani Tanga.
Mafunzo hayo muhimu yanalenga kuimarisha uwezo na weledi wa maofisa hao wanaosimamia usalama wakati wa michezo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, mpango huo wa mafunzo utahusisha Maofisa wa Ulinzi na Usalama wa Mikoa pamoja na wale wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship, First League, na Ligi Kuu ya Wanawake.
Kutokana na umuhimu wa nafasi hizo, TFF imezitaka klabu zote zinazohusika kuwasilisha majina ya wawakilishi wao watakaoshiriki mafunzo hayo kabla ya Agosti 3, 2026, kupitia barua pepe rasmi au kwa kuwasiliana moja kwa moja na Mratibu wa Mafunzo, huku ada ya ushiriki ikiwa ni shilingi 200,000 kwa kila mshiriki.
Ili kuhakikisha ubora na ufanisi wa ulinzi viwanjani, TFF imeweka wazi sifa za kuzingatia katika uteuzi wa ofisa atakayeshiriki, ambapo inatakikana awe na historia ya kufanya kazi ya ulinzi na usalama, amepitia mafunzo ya askari, au awe askari mstaafu.
Vilevile, mteule anapaswa kuwa mtawala au mwanafamilia wa mpira wa miguu, mtu anayeaminika, na mwenye moyo wa kujituma, huku upande wa Mkoa ukitakiwa kuzingatia weledi, uzito, na hadhi ya nafasi hiyo wakati wa kupendekeza majina.

Post a Comment