Serikali yatangaza Fursa ya mafunzo ya uyaya Qatar




Na Rahel Pallangyo

Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, ikishirikiana na Wakala Almaha Travel and Tours Company Limited pamoja na Khalid Islamic Foundation, imetangaza nafasi 40 za mafunzo ya uyaya nchini Qatar.

Mafunzo hayo yatatolewa na Chuo cha Mafunzo ya Uyaya nchini humo cha Qatar Nanny Academy. 

Fursa hii inawahusu wanawake wenye umri kuanzia miaka 20 hadi 40, wenye tabia njema, elimu ya sekondari au thanawi (kiwango cha sekondari katika dini ya Kiislamu), pamoja na uwezo wa kuongeza na kuandika lugha ya Kiarabu. 

Mafunzo haya yatachukua muda wa miezi 12, ambapo gharama za mafunzo, visa, tiketi ya ndege, malazi, na chakula zitagharamiwa na chuo husika, wakati gharama za matibabu kwa kipindi chote zitakuwa chini ya mwajiri.

Aidha, washiriki watalipwa posho ya kujikimu ya Riyal 500 za Qatar (QAR 500) kwa mwezi, sawa na takribani shilingi 360,000 za Kitanzania, na baada ya kuhitimu mafunzo hayo kwa mafanikio watapatiwa ajira nchini Qatar kwa mkataba wa miaka miwili.  

kwa mujibu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Waziri Mkuu,Wizara ya kazi, Ajira na Mahusiano maombi yote yanatakiwa yatumwe kupitia barua pepe ya info@almaha.co.tz huku yakinakiliwa kwenda kwa abdulaziz-kif@bakhresa.com kuanzia leo Julai 27 hadi  Julai 31 2026.

Aidha tangazo hilo limesema baada ya kutuma maombi hayo, waombaji wanatakiwa kujisajili kupitia tovuti ya https://jobs.kazi.go.tz. 

Usaili wa nafasi hizo utafanyika Agosti 3, 2026, ambapo wakazi wa Dar es Salaam watafanyia katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano iliyoko mkabala na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwenye Barabara ya Bibi Titi Mohamed, na wale walioko nje ya Dar es Salaam watafanya kwa mtandao

No comments