Tanzania ni Imara: Watanzania Wahimizwa Kupuuza Chokochoko za BBC



Serikali ya Tanzania, kupitia Idara ya Habari-MAELEZO, imetoa wito kwa Watanzania wote kuwa makini na kupuuza chokochoko zinazofanywa dhidi ya nchi kupitia vyombo vya habari vya kimataifa na mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Serikali imesikitishwa na makala iliyochapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia kipindi cha "BBC Africa Eye," ikielezea kuwa makala hiyo ina upande mmoja, haina ushahidi thabiti, na ina mwelekeo wa kuchafua heshima ya Tanzania kimataifa.

Wito huo wa Serikali unakuja wakati ambapo mijadala kuhusu siasa za upinzani nchini imeshika kasi, hasa kufuatia makala hiyo ya BBC inayomlenga mwanasiasa Tundu Lissu.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema ni vyema kuangalia taswira kamili ya mwanasiasa huyo badala ya kuzingatia kadhia zake pekee.

Katika makala ya maoni yenye kichwa "Beyond the Suffering: What the BBC Documentary Missed About Tundu Lissu and What Tanzanian Women See," mwandishi Norah Msemwa anahoji kuwa Makala hiyo ya BBC ilishindwa kutoa picha kamili ya mwanasiasa huyo kwa kuacha mambo muhimu kuhusu mbinu zake za kisiasa.

Kwa nini Lissu anagongana na Serikali?

Uchambuzi huo unaonesha kuwa tofauti na wanasiasa wengi wa upinzani nchini, Tundu Lissu amejijengea sifa ya kuwa mwanasiasa anayependelea makabiliano badala ya maridhiano. Mwandishi anabainisha kuwa Lissu amekuwa akichagua njia ya mapambano magumu badala ya ushirikiano, jambo ambalo limekuwa likimuingiza mara kwa mara katika migogoro ya kisheria na serikali kwa miongo kadhaa.

Baada ya kurejea nchini, Lissu alibadilisha mwelekeo wa chama chake kwa kushinda uongozi wa ndani mnamo Januari 2025, akijinadi kwa sera ya kutaka mapambano makali na kukataa "kuambiana mambo ya maridhiano".

Aidha, makala hiyo inabainisha kuwa migogoro yake na serikali imechochewa pia na hatua kama vile kampeni ya "No Reforms, No Election," kukataa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, na msimamo wake wa kutaka mapambano badala ya mazungumzo.

Wakati Serikali ikiendelea kusimamia misingi ya amani, umoja, na mshikamano wa Watanzania wote huku ikitekeleza afua za kukabiliana na changamoto za kisiasa, kiuchumi, na kijamii, wachambuzi wanatoa rai kuwa ni muhimu kwa jamii kuelewa kuwa demokrasia haijengwi kwa ibada ya mtu binafsi.

Ni dhahiri kuwa Tanzania inahitaji viongozi wa upinzani wanaoweza kupinga mamlaka kwa uwajibikaji, na serikali inayojibu hoja kupitia taasisi, badala ya kutegemea mihemko ya kisiasa inayoweza kuleta mgawanyiko.

No comments