Taifa Laungana Kuadhimisha Siku ya Mashujaa Kitaifa




TAIFA leo Julai 25 linaungana katika kumbukumbu maalum ya Siku ya Mashujaa katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, ambapo viongozi, wananchi, na vyombo vya ulinzi na usalama vinashiriki kwa pamoja kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliopigania uhuru na rasilimali za nchi. 

Maadhimisho haya ya kitaifa, yataoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yanatoa fursa adhimu ya kutafakari mchango mkubwa wa mashujaa wa historia ya Tanzania, wakiwemo wale waliopigania uhuru dhidi ya ukoloni, mashujaa wa Vita vya Majimaji, na wale waliopoteza maisha wakilinda mipaka ya nchi katika Vita ya Kagera na migogoro mingine ya kulinda amani iliyohusisha taifa. 

Shughuli rasmi za maadhimisho hayo zilianza tangu usiku wa kuamkia Julai 25, 2026, kwa viongozi wa ngazi ya mkoa na wananchi kuwasili kwenye eneo la mnara chini ya uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambaye aliongoza gwaride dogo la Jeshi la Polisi kuwasha Mwenge wa Mashujaa saa sita kasoro usiku kabla ya rasmi kutoa nafasi kwa matukio ya mchana. 

Mapema kuanzia saa mbili asubuhi ya Julai 25, wageni waalikwa, vikosi vya burudani vya JKT Makutupora Jazz Band, na gwaride maalum litaingia uwanjani na kuanza kupokea viongozi wakuu wa kitaifa kabla ya kupokelewa kwa Mkuu wa Nchi saa tatu kamili asubuhi. 

Katika kilele cha tukio hilo la kitaifa uwanjani hapo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atapokelewa na Mkuu wa Majeshi na kusimama kwa ajili ya heshima ya kitaifa iliyojumuisha kupigwa kwa Wimbo wa Taifa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikifuatiwa na kikundi cha buruji kupiga "Last Post", upigaji wa mizinga miwili, na dakika moja ya ukimya ya maombolezo kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa wote waliotangulia mbele za haki. 

Baada ya hapo, viongozi wakuu wakiongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wataweka silaha za asili na shada la maua kwenye Mnara wa Mashujaa, ambapo Rais ataweka mkuki na ngao, Mkuu wa Majeshi ataweka sime, kiongozi wa mabalozi ataweka shada la maua, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma ataweka upinde na mshale, na Shujaa wa Taifa ataweka shoka, ikifuatiwa na dua na sala kutoka viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo kutoka BAKWATA, CCT, na TEC. 

Maadhimisho haya hayakamiliki bila kutoa fursa kwa jamii kutambua kuwa amani na uhuru wa sasa vimetokana na damu na jasho la mababu na askari wetu waliojitoa muhanga katika vita mbalimbali vya kihistoria kulinda ardhi ya Tanzania, kuanzia mapambano ya kupinga wakoloni wakati wa Vita vya Majimaji hadi kujitolea mhanga katika Vita ya Kagera na ukombozi wa bara la Afrika. 

Kutokana na ratiba hiyo iliyopangiliwa kwa ustadi mkubwa na Kurugenzi ya Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa, shughuli zitahitimishwa rasmi usiku wa manane kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma kuzima Mwenge wa Mashujaa, ikiashiria kukamilika kwa ibada na shamrashamra za kuwaenzi mashujaa hao na kuwakumbusha Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja, na mshikamano uliowekwa na misingi ya mashujaa wa taifa hili.  

No comments