TORRES AIPA HISPANIA KOMBE LA DUNIA



Hispania usiku wa kuamkia leo imetawazwa kuwa mabingwa wa dunia kwa mara ya pili katika historia yao baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Argentina katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia uliochezwa kwenye Uwanja wa New York New Jersey, uliopo East Rutherford, New Jersey. 

Bao pekee na la kihistoria lililofungwa na mshambuliaji wa alioyetokea benchi Ferran Torres katika dakika ya 106  lilitosha kuinyamazisha Argentina na kurejesha taji hilo mikononi mwa Waspaniola baada ya mchezo  mgumu na wenye ushindani mkubwa. Hadi Refa anapuliza filimbi dakika ya 90 milango ilikuwa haijafunguka.



Mchezo huo uliowakutanisha mabingwa wa Ulaya na Amerika Kusini ulianza kwa kasi huku Hispania ikitawala mpira tangu kipindi cha kwanza kupitia nyota wao chipukizi Lamine Yamal na Dani Olmo, ingawa ukuta mgumu wa Argentina uliokuwa chini ya kipa stadi Emiliano Martinez ulisimama kidete kuokoa michomo kadhaa ya hatari. 

Argentina ilipata pigo baada ya mabeki wake wawili wa kati, Lisandro Martinez na Facundo Medina, kupata majeraha na kulazimika kutoka uwanjani, wakati kwa upande wa Hispania mashambulizi yaliendelea kupitia kwa Torres, Pau Cubarsi na mwenzake Pedri, huku kipa Martinez akiendelea kufanya kazi ya ziada kuwanyima mabao Hispania hadi dakika 90 zikakamilika.



Kipindi cha nyongeza cha dakika 30 kilianza huku Argentina ikiwa pungufu uwanjani baada ya kiungo wao Enzo Fernandez kuonyeshwa kadi ya pili ya njano mwishoni mwa muda wa kawaida kufuatia kumchezea madhambi beki Pau Cubarsi. Hispania ilitumia vizuri upungufu huo katika dakika ya 106 pale ambapo Pedro Porro alipopiga krosi safi iliyopigwa kichwa cha chini na Nico Williams kwenye eneo la mbali, kabla ya Ferran Torres kuuwahi mpira huo na kuachia kombora kali lililojaa moja kwa moja kwenye nyavu na kuwasha shangwe kubwa kwa mashabiki wa La Roja waliokuwa wakishuhudia ushindi huo mtamu.

Ushindi huo uliambatana na kuvunjwa kwa rekodi ya kipekee kwa Hispania kutwaa ubingwa huo kwa kuruhusu bao moja pekee katika michuano yote, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na timu iliyotwaa Kombe la Dunia, huku kipa wao Unai Simon akiweka rekodi ya kulinda lango lake bila kuruhusu bao katika mechi saba. 



Nyota chipukizi Lamine Yamal na Pau Cubarsi, wote wakiwa na umri wa miaka 19, wameungana na magwiji kama Pele na Kylian Mbappe kushinda taji hili wakiwa wangali vijana wadogo, wakati kocha wao Luis de la Fuente, mwenye umri wa miaka 65, akiweka rekodi ya kuwa kocha mzee zaidi kutwaa kombe hilo.

Akizungumza baada ya mchezo huo uliovuta hisia za mamilioni ya watu duniani, shujaa wa usiku huo Ferran Torres alieleza kuwa lile lilikuwa tukio kuu na lenye furaha isiyo kifani katika maisha yake yote ya soka.

Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente, aliwapongeza vijana wake kwa kuonyesha moyo wa familia na kupambana hadi dakika za mwisho licha ya kukutana na ugumu kutoka kwa kipa Dibu Martinez, huku kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, akikiri wazi kuwa Hispania ilikuwa bora zaidi uwanjani huku akimpongeza nahodha wake Lionel Messi kwa rekodi yake ya kipekee ya kucheza fainali tatu za Kombe la Dunia.

No comments