MAMA SALMA KIKWETE AHIMIZA KISWAHILI KATIKA BUNGE LA UINGEREZA




Balozi wa Kiswahili Barani Afrika, Mheshimiwa Salma Kikwete, amesisitiza kuwa lugha ya Kiswahili ni chombo muhimu cha kuimarisha mshikamano, utamaduni, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi duniani.

Aidha amebainisha kuwa kuendelea kwa matumizi yake katika majukwaa ya kimataifa ni ushahidi wa nafasi yake kubwa katika kuunganisha mataifa na tamaduni tofauti. 

Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni katika tukio hilo maalum la maadhimisho ya Siku ya Kiswahili lililofanyika katika Bunge la Uingereza (House of Lords) jijini London kwa mwaliko wa Mheshimiwa Lord Paul Boateng, ambaye ni Mjumbe wa Baraza hilo la Juu.









Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanadiplomasia, wabunge, wadau wa elimu pamoja na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kutoka mataifa mengi, ambapo ilipambwa pia na ushiriki wa Mabalozi wa nchi za Afrika nchini Uingereza wakiongozwa na Amidi wa Mabalozi hao, Mheshimiwa Christiane Katsande.

Uwepo wao uliakisi umoja wa bara hilo katika kuipa hadhi lugha ya Kiswahili. Sambamba na hilo, uwepo wa mwanamuziki mashuhuri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kanda Bongo Man, uliongeza msisimko na kutambua mchango mkubwa wa wasanii wa Afrika katika kueneza lugha hiyo kupitia muziki uliovuka mipaka na kufikia hadhira ya kimataifa. 

Katika hotuba yake Mheshimiwa Salma Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete,alipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wadau wengine kwa juhudi zao thabiti za kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya Kiswahili katika nyanja za elimu, biashara, diplomasia, na teknolojia, akisisitiza kuwa lugha hiyo ni sehemu adhimu ya urithi wa Afrika na nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.



No comments