Ziara ya Rais Samia Nchini Urusi Yawaacha Wanafunzi wa Kitanzania Wakijivunia Diplomasia ya Juu na Fursa za Kiteknolojia
Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Petersburg, Urusi
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imepokelewa kwa furaha na fahari kubwa na jumuiya ya wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini humo, ambao wameeleza kuwa wana kila sababu ya kujivunia uongozi wake.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Kitanzania nchini Urusi (TASCORU), ambaye pia ni mwanafunzi anayesomea masuala ya madini (Mining) katika Chuo Kikuu cha Urafiki RUDN, Jofrey Mashauri amebainisha kuwa ujio wa kiongozi mkuu wa nchi ni sehemu ya historia isiyofutika ambayo imeacha alama kubwa mioyoni mwao.
Wanafunzi hao wamesisitiza kuwa Watanzania nyumbani wanapaswa kuelewa na kuthamini sifa njema ambayo taifa inaendelea kuipata kimataifa, kwani kupata mwaliko rasmi wa kutembelea nchi kubwa kama Urusi si jambo dogo au la kubeza hata kidogo.
Urusi ikiwa ni moja ya mataifa yenye nguvu kubwa duniani, hususani katika nyanja za teknolojia na uzalishaji wa viwandani, ziara hii inatajwa kuwa na uzito mkubwa wa kimkakati.
Wameongeza kuwa uongozi wa Rais Samia unazidi kuiweka Tanzania katika eneo zuri la kidiplomasia duniani kote, huku ukifungua njia na fursa mbalimbali kwa vijana wanaotafuta maarifa na maendeleo.
Kuhusu maisha yao ya kimasomo, shirikisho hilo limeeleza kuwa Urusi ina mazingira mazuri ya kuishi na mfumo wa elimu ulio bora sana.
Kwa mfano, katika Chuo Kikuu cha RUDN pekee, kuna jumla ya wanafunzi wa Kitanzania 96 ambao wanajifunza fani mbalimbali za kimkakati zikiwemo sheria, uhandisi, udaktari, sayansi ya nyuklia, ujenzi, na masuala ya madini.
Pamoja na uzuri wa maisha hayo na ukweli kwamba gharama za vyakula nchini humo si kubwa, wanafunzi hao wamebainisha kuwa kama wakipata ongezeko au upatikanaji mzuri wa fedha za kujikimu kutoka nyumbani kama wenzao, maisha yao ya kimasomo yatakuwa bora na yenye tija zaidi.
Wanafunzi hao pia wamemwagia sifa kiongozi wa uwakilishi wa kidiplomasia wa Tanzania nchini humo, Balozi Frederick Kibuta, kwa kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa raia na wanafunzi wote wa Kitanzania waliopo Urusi.
Wamebainisha kuwa malezi na ushirikiano wa karibu kutoka ubalozini umekuwa nguzo muhimu inayowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kimasomo kwa amani na utulivu, huku wakijisikia wakiwa salama kama wapo nyumbani.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi una historia ndefu iliyoasisiwa tangu enzi za Vita Baridi, ambapo Umoja wa Kisovieti (USSR) ulikuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Tanganyika na baadaye Tanzania.
Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano huu umeendelea kuimarika kutoka kwenye masuala ya kisiasa na kiulinzi pekee na kugusa sekta za kiuchumi, biashara, na utamaduni.
Urusi imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya rasilimali watu nchini Tanzania kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Kitanzania katika fani ngumu za kisayansi, hatua inayosaidia kuziba mapengo ya wataalamu katika sekta za nishati, afya, na miundombinu hapa nchini.
Post a Comment