RAIS SAMIA: TANZANIA HAIFUNGAMANI NA UPANDE WOWOTE, INASAKA FURSA ZA KIUCHUMI KILA PEMBE YA DUNIA



Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Petersburg, Urusi

Ulimwengu wa sasa wa diplomasia ya kijiografia unatawaliwa na ushindani mkubwa wa nguvu za kisiasa na kiuchumi kati ya mataifa makubwa ya Magharibi na yale ya Mashariki. 

Katika mazingira haya, mataifa yanayoendelea mara nyingi hujikuta yakitazamwa kwa darubini ya shaka pale yanapochukua hatua za kimkakati kupanua wigo wa washirika wao wa kimaendeleo. 

Ziara ya hivi karibuni ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imezua minong'ono na hisia mbalimbali miongoni mwa wachambuzi wa mambo, wengi wao wakihofia kuwa huenda Tanzania sasa inabadili mwelekeo wake wa sera ya mambo ya nje kwa kuitupa mkono Magharibi na kugeukia upande wa Mashariki. 

Hofu hii haina msingi wowote, kwani majibu thabiti na ya kizalendo aliyoyatoa Rais Samia mbele ya waandishi wa habari pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa ya Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) nchini Urusi, yanadhihirisha ukomavu wa diplomasia ya Tanzania inayojali maslahi ya taifa kwanza kabisa.

Katika mazungumzo hayo maalum yaliyowashirikisha waandishi wa habari 13 walioambatana naye, akiwemo mwakilishi kutoka Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN), Rais Samia alikuwa wazi na alinyoosha maelezo bila kusita. 

Alifafanua kuwa Tanzania haihamishi nguvu zake kutoka upande mmoja kwenda mwingine, bali inaongeza wigo wa washirika ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi yanatimizwa kwa faida ya wananchi wake. 

Hii ina maana kwamba wale wote wenye hofu au mashaka kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Urusi wanapaswa kuondoa shaka hiyo mara moja, kwani serikali haifuati mtu au upande wowote wa kiitikadi, bali inafuata yeyote mwenye nia njema ya kushirikiana katika kuinua maisha ya Watanzania.

Msimamo huu wa Rais Samia si jambo geni wala la kubahatisha, bali ni muendelezo wa misingi imara ya kihistoria iliyowekwa na Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Miaka 57 iliyopita, Mwalimu Nyerere alipotembelea Urusi (wakati huo ikiwa Muungano wa Sovieti), alitamka maneno yaleyale yanayosikika leo kutoka kwa Rais Samia: kwamba Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote. Mwalimu alisisitiza kuwa Tanzania itajichanganya na marafiki zake kwa jinsi marafiki hao wanavyotaka kuwa na Tanzania, mradi tu hawataingilia uhuru na mamlaka ya nchi. Falsafa hiyo ya kihistoria ndiyo inayomwongoza Rais Samia hadi leo katika ulimwengu huu unaozidi kuwa na vitovu vingi vya nguvu ya kiuchumi na kiteknolojia.

Sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote (Non-Aligned Policy) imekuwa silaha kuu ya kulinda uhuru wa Tanzania wa kufanya maamuzi ya kimkakati. Katika kile kinachoitwa Diplomasia ya Maslahi ya Kitaifa (National-Interest Diplomacy), kigezo kikuu cha kupima ubora wa uhusiano wa kimataifa si itikadi za kisiasa, bali ni mchango gani uhusiano huo unaingiza katika uchumi wa nchi, ajira kwa vijana, na uhamishaji wa teknolojia. 

Rais Samia alifafanua kuwa ziara yake nchini Urusi ilikuja na maombi saba ya kimkakati kutoka Tanzania, na wenyeji wao wa Urusi wakavutiwa kiasi cha kuongeza maombi mengine mawili na kufanya jumla ya maeneo tisa ya ushirikiano. Hii inadhihirisha kuwa pande zote mbili zinazungumza lugha moja inayolenga ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Ili kuelewa kwa nini Tanzania inapaswa kuendelea kushirikiana na Urusi pamoja na ulimwengu mzima, ni lazima kuangalia uwiano wa washirika wetu duniani kote. 

Serikali ya Awamu ya Sita haijafunga milango kwa mataifa ya Magharibi; badala yake washirika wetu wa kitamaduni wanaendelea kuwa nguzo muhimu. Kwa mfano, Marekani bado ni mshirika mkubwa sana wa kiuchumi na kibiashara nchini Tanzania, ikiongoza katika kuleta watalii wengi na kuwekeza kupitia kampuni kubwa zaidi ya 500 zilizopo nchini, hususan katika sekta ya madini na uwekezaji mbalimbali wa kimkakati. Vivyo hivyo, mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa washirika  wakuu katika biashara na utoaji wa misaada pamoja na uwezeshaji wa kifedha. Uhusiano huu wa karibu na Magharibi haujatikisika, na unazidi kuimarika kila uchao.

Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kunufaika na uhusiano mkubwa na mataifa ya Asia. China imekuwa mshirika  mkuu wa kihistoria na wa sasa katika kuwezesha miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, huku India nayo ikiwa miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara .

Japan haikuachwa nyuma, kwani imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta za nishati, elimu, na ujenzi wa miundombinu ya kijamii. Hata mataifa mengine kama Australia, Uingereza, na Ufaransa yamekuwa yakija nchini kwa kasi kupitia mipango mbalimbali kama vile mpango wa Matei wa Ufaransa ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi. 

Kwa mtazamo huu, Urusi inaingia kama mshirika mwingine muhimu wa kimkakati baada ya Tanzania kumaliza changamoto zilizotokana na masharti magumu ya mabadiliko ya kiuchumi ya Benki ya Dunia katika miaka ya 1980, ambayo wakati huo yalilazimu Tanzania kuangalia upande mmoja tu wa mlango.

Ni dhahiri kuwa Diplomasia ya sasa ya Tanzania inatawaliwa na ukomavu na uhuru wa kuchagua. Kama alivyowahi kunukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuhusu methali maarufu ya kiuchumi: "Tanzania haihitaji kujua rangi ya paka, mradi tu paka huyo ana uwezo wa kukamata panya." 

Maneno haya yana maana kwamba Tanzania haichagui wala haibagui mshirika kwa kuangalia sura au mfumo wake wa kisiasa, bali inaangalia uwezo na utayari wa mshirika huyo kushirikiana nayo katika kutatua changamoto za umaskini na kukuza uchumi. Kila taifa linaloheshimu mamlaka ya Tanzania na liko tayari kuchangia katika ustawi linakaribishwa kwa mikono miwili.

Mkakati huu wa kutafuta washirika wengi kwa wakati mmoja una umuhimu mkubwa sana katika kulinda usalama wa kiuchumi wa Tanzania. Hakika kuweka mayai yote kwenye kikapu kimoja ni hatari kubwa katika ulimwengu wa sasa uliopasuka kutokana na vikwazo vya kiuchumi na migogoro ya kikanda. Kuwa na washirika mbalimbali kunatoa nguvu kubwa ya majadiliano (bargaining power) kwenye meza za kimataifa, kwani hatutegemei chanzo kimoja tu cha mitaji au teknolojia. Kama soko moja likiyumba au kukiwa na mabadiliko ya kisiasa upande mmoja, Tanzania inaweza kuendelea kusonga mbele kwa kutumia milango mingine iliyo wazi.

Kwa kuwa, dira yetu ya maendeleo ya taifa ya 2050 ndiyo dira kuu inayoongoza Tanzania hivi sasa ni vyema kama taifa kutumia diplomasia ya kiuchumi kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, lengo likiwa ni kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa na kufikia thamani ya uchumi wa dola bilioni 1,000 (trilioni moja) ifikapo mwishoni mwa utekelezaji wake. 

Ili kufikia lengo hili kubwa la kihistoria, serikali inahitaji mitaji mikubwa, miundombinu ya kisasa, na teknolojia ya hali ya juu kutoka kila kona ya dunia. Tanzania haiwezi kufikia malengo hayo makubwa kwa kujifungia milango au kwa kuchagua upande mmoja wa kidunia. Ndiyo maana Rais Samia anapiga hatua kwa ujasiri, akifungua milango kila mahali—iwe ni Washington, Beijing, Brussels, au Moscow—kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa yanalindwa na fursa za kiuchumi zinawafikia wananchi wote.

mwisho

No comments