Ndoto ya Miaka Mingi ya Kuwa Mama Yatimia
Machozi ya miaka mingi, maswali yasiyo na majibu kutoka kwa jamii, na safari ndefu ya matibabu hatimaye, Malkia wa filamu na mwanamitindo mashuhuri nchini, Wema Sepetu na mpenzi wake , Oscar Lelo maarufu kama 'Whozu', wamemkaribisha mtoto wao wa kwanza wa kiume.
Mtoto huyo amekuja ndani ya miaka minne ya uhusiano wa wawili hao na kutikisa kwa namna yake mitandao ya kijamii tangu kuchapishwa kwa picha ya mguu wa mtoto huyo, ikisindikizwa na maneno mazito ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa muujiza huo mkubwa uliotokea tarehe 12 ya mwezi huu.
Kwa Wema, ujio wa mtoto huyu si tu baraka, bali ni ushindi mkubwa dhidi ya majaribu mazito aliyopitia maishani mwake. Safari yake ya kutafuta mtoto imekuwa ya wazi na iliyojaa maumivu, ikiwemo kufanyiwa upasuaji mkubwa nchini India mwaka 2018 wa kuondoa uvimbe kwenye ovari, pamoja na kukumbana na dhoruba ya kupoteza ujauzito huko nyuma.
Whozu yeye anasherehekea kupata mtoto wake wa pili baada ya yule wa kwanza aliyemzaa na Tunda. Kwa Wema hii ni mara yake ya kwanza kuonja ladha ya kuitwa mama, jambo ambalo lilimfanya kuandika kwa hisia akisema "Ooh! This is God". Whozu naye hakusita kuonyesha ukuu wa Mungu kwa kueleza kuwa mipango ya wanadamu haiwezi kushinda kudra za muumba, huku akitangaza siku hiyo kama Sikukuu .
Habari hii imezua mtikisiko mkubwa wa furaha mitandaoni, huku maelfu ya mashabiki na wadau wa burudani wakifurika kwenye kurasa zao kutoa pongezi za dhati. Sehemu ya maoni iligeuka kuwa uwanja wa shangwe ambapo mashabiki walionyesha kuguswa kwa dhati na ushindi wa Wema, wengi wao wakisisitiza kuwa mtoto huyo anapaswa kuitwa "Miracle" yaani Muujiza, kutokana na mapito magumu aliyopitia mama yake.
Mashabiki walimpongeza Whozu kwa kuwa mwanaume aliyesimama imara na kuwaziba mdomo wale wote waliokuwa wakihoji juu ya uhusiano wao, huku wengine wakimtania kwa maneno ya kichokozi kuwa ameweza "kutetema kwenye mechi ngumu" na kufanya vizuri kama mtaalamu wa mipira ya adhabu.
Mazingira ya Instagram yamechangamka kupita kiasi, huku mashabiki wakikiri kuwa wameshindwa kulala kwa ajili ya kufuatilia kila updates ya mtoto huyo ambaye amekuja kama mfalme aliyebarikiwa.
Hisia za upendo zilitawala kila kona, wengine wakipiga kelele za furaha mtandaoni na kueleza jinsi mioyo yao ilivyobubujikwa na amani kuona Wema hatimaye ameshika mtoto wake mikononi mwake.
Ni wazi kuwa kuzaliwa kwa mtoto huyu kumefungua ukurasa mpya na wa kihistoria, si tu kwa Wema na Whozu kama wazazi, bali pia kwa mamilioni ya mashabiki ambao wamemshuhudia staa wao akitoka kwenye simanzi ya miaka mingi na kuingia kwenye nuru ya kuitwa mama.





Post a Comment