Dira ya Taifa kupima ukuaji michezo, sanaa na utamaduni




SEKTA ya michezo na sanaa imepewa viashiria tisa vitakavyopima ukuaji wake katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itakayoanza kutekelezwa Julai Mosi, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Utekelezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema taifa linaanza utekelezaji wa dira hiyo likiwa na nyenzo zote muhimu. 

Alisema Tume ya Taifa ya Mipango imeidhinisha miongozo minne itakayotumika kusimamia utekelezaji wa Dira ya 2050 ambayo ni Mwongozo wa Kitaifa wa Mipango, Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo, Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050 wa miaka mitano 2026/2027-2030/2031.

Mkumbo alisema sekta ya michezo na sanaa imetambuliwa rasmi kama nguzo muhimu ya kiuchumi na kijamii na ili kuhakikisha sekta hizo zinakuwa kitovu cha utamaduni na uchumi, serikali inatumia viashiria vifuatavyo kama vipimo vya mafanikio. 

Alisema moja ni sekta hiyo kuwa uchumi na ajira ambapo dira itapima kiasi cha fedha kinachozalishwa moja kwa moja na sekta ya michezo, ubunifu, burudani na sanaa.

Kadhalika kupima idadi ya vijana walioajiriwa rasmi katika tasnia hizi (kama vile wanamichezo, waigizaji, wanamuziki, wabunifu na maudhui ya kidijiti) na kufuatilia ongezeko la mapato yanayotokana na mauzo ya kazi za sanaa nje ya nchi na utalii wa kitamaduni na michezo nje ya nchi. 

Pia, maendeleo ya vipaji na miundombinu ambapo ni kujenga vituo vya ukuzaji vipaji na kupima utendaji wa vituo vya michezo na sanaa ili kukuza vipaji vya watoto na vijana hadi kufikia viwango vya kimataifa, upimaji wa upatikanaji, ubora, na usambazaji wa viwanja vya kisasa vya michezo na kumbi za sanaa nchi nzima.

No comments